May 14, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bajeti ya Trilioni 2.4 uboreshaji Elimu yapitishwa Bungeni

Na Joyce Kasiki, Timesmajira online,Dodoma

BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha bajeti ya Shilingi trilioni 2.44 kwa ajili ya kuiwezesha Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kutekeleza majukumu yake kwa mwaka wa fedha 2025 huku ikiahidi kuendelea kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia pamoja na kuongeza idadi ya walimu nchini.

Akizungumza Mei 13,2025 Bungeni jijini Dodoma wakati wa kuhitimisha mjadala wa bajeti hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI imejipanga kuboresha mazingira ya kufundishia kwa kujenga madarasa, kutoa vifaa vya kujifunzia na kuajiri walimu wapya.

Wakati wa mjadala wa bajeti hiyo, baadhi ya Wabunge wameipongeza Serikali kwa jitihada kubwa katika sekta ya elimu, hususan kuanzishwa kwa mitaala mipya na kuboresha mazingira ya kujifunzia kuanzia ngazi ya awali hadi vyuo vikuu. Pia walitoa ushauri wa namna ya kuimarisha sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Mbunge wa Nanyamba, Abdallah Chikota, ameishauri Wizara ya Elimu kuwapatia mafunzo walimu waliopo kazini ili kuongeza ufanisi wao na kuwapa maarifa mapya. Alizitaja faida tano za mafunzo hayo kuwa ni kukuza utendaji, kuongeza maarifa, kuboresha uhusiano kazini, kuimarisha uelewa wa kazi na kuongeza kipato cha mtumishi.

Mbunge wa Viti Maalum, Thea Ntara, ameipongeza Serikali kwa kuongeza bajeti ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, hatua iliyosaidia kupunguza malalamiko kuhusu ukosefu wa mikopo.

“Hivi sasa tunaona wanafunzi wengi sana wanapata mikopo na hakuna malalamiko katika eneo hilo,” alisisitiza Ntara.

Pia ameipongeza uanzishwaji wa mitaala mipya licha ya changamoto zake, na kuitaka Wizara kuendelea kutoa elimu kuhusu mitaala hiyo hasa katika eneo la Mafunzo ya Amali.

“Kila mabadiliko huja na changamoto zake. Ni lazima Serikali ikabiliane nazo. Elimu ya Amali iendelee kufafanuliwa kwa jamii ili kuelewa faida zake na kuwahamasisha wazazi kuwapeleka watoto kusomea fani hizo,” amesema Ntara.

Kwa upande wake, Mbunge wa Singida Mjini, Musa Sima, aliishauri Wizara hiyo kuzingatia maeneo matano muhimu katika utekelezaji wa bajeti hiyo, likiwemo kuongeza fedha kwa elimu ya ufundi ili kuwapa vijana ujuzi wa kujitegemea.

Aidha, amesisitiza haja ya kuwa na mpango maalum wa kuwaajiri walimu wa kujitolea, sambamba na maandalizi ya mapema kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2028 ambao idadi yao inatarajiwa kuongezeka.

Katika hatua nyingine, Sima alihoji kuhusu bajeti ya Sh bilioni 200 iliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa vyuo 64 vya ufundi pamoja na chuo kimoja cha mkoa wa Songwe, huku bajeti ya vifaa na walimu ikiwa haijawekwa wazi.

Pia alishauri Chuo cha Teknolojia cha Dar es Salaam (DIT) kujielekeza zaidi kwenye matumizi ya satelaiti kwa ukusanyaji wa taarifa za kilimo na mazingira badala ya kuzingatia taarifa za wanyamapori pekee.

Mbunge huyo ameisisitiza Serikali kuongeza ajira kwa walimu wapya ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi kutokana na mabadiliko ya sera ya elimu.