*Wadau wasisitiza elimu ndio msingi wa mabadiliko ya matumizi ya nishati safi
*EWURA yasisitiza mabadiliko yanahitaji mpango wa muda mrefu na elimu endelevu
Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online – Mwanza
Wadau wa sekta ndogo ya mafuta mkoani Mwanza wametoa wito kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuongeza juhudi za uelimishaji juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, hususani katika maeneo ya vijijini.
Wito huo umetolewa Mei 13, 2025, wakati wa semina ya siku moja ya wadau wa sekta ndogo ya mafuta iliyofanyika jijini Mwanza, iliyoandaliwa na EWURA.

Wakizungumza katika semina hiyo, wadau wamesema elimu ni msingi wa mabadiliko ya mtazamo kutoka matumizi ya nishati chafu kama kuni na mkaa kuelekea matumizi ya gesi na vyanzo vingine vya nishati safi.
Ofisa Masoko wa kampuni ya Kayonza LTD Oryx, Joaness Kashaga, amesema kuwa watu wengi waishio vijijini bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu faida na matumizi ya nishati safi ya kupikia.Amesisitiza kuwa kufikia lengo la serikali la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ifikapo 2034 kunahitaji uwekezaji elimu kwa jamii.
“Elimu ndio mkombozi wa wananchi kuacha matumizi ya nishati chafu kama mkaa,hivyo nasisitiza EWURA kutisaidia kutoa elimu na kampeni za kuhamasisha na kuwajengea uelewa wananchi hususani wa vijijini ili waondokane na matumizi ya nishati chafu,”amesema Kashaga.
Naye Ofisa Biashara kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, Evalina Ndeji,amewataka washiriki wa semina hiyo kupeleka elimu waliyoipata kwa wananchi, hasa wanawake wanaopika wakiwemo mama ntilie ili waondokane na matumizi ya nishati chafu na kufikia malengo hayo ya miaka 10.
Pia ametoa wito kwa serikali kupitia EWURA kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa wananchi hususani wa vijijini juu ya matumizi ya nishati safi,kwani wengi wao uelewa bado ni mdogo huku mfano hali ni eneo analofanyia kazi.Pia kuona namna ya kupunguza gharama za kujaza gesi ili kuwawezesha wanawake wa kipato cha chini kutumia nishati safi.
Kwa upande wake, Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, George Mhina,amesema mabadiliko ya matumizi ya nishati si ya mwaka mmoja, bali yanahitaji mpango wa muda mrefu unaojumuisha elimu endelevu na ushirikiano wa wadau wote, wakiwemo waandishi wa habari.
“Suala la kubadili mtazamo wa wananchi kutoka kutumia nishati chafu ya mkaa na kuni siyo la muda mfupi, linahitaji muda na sasa kamati mbalimbali zimeisha undwa za kuhakikisha huduma na elimu inawafikia wananchi.Pia nishati safi siyo gesi tu kwa sasa kuna mkaa wa kisasa ambao ni rafiki kwa mazingira,”.

Mhina,amefafanua kuwa safari hiyo ya miaka 10 (2024-2034), ya asilimia 80 iwe inatumia nishati safi ya kupikia,ilianza rasmi mwaka jana, ikiwa na mikakati ya pamoja ya wizara, taasisi na wadau mbalimbali, wakiwemo TAMISEMI, Wizara ya Nishati na Wizara ya Fedha, kuhakikisha elimu inatolewa, vifaa vinapatikana, na sera zinazowezesha matumizi ya nishati safi zinaimarishwa.


More Stories
Maonesho ya 49 ya Sabasaba kuanza kufanyika Juni 28
Upanuzi wa Kituo cha Kupoza Umeme Mbagala mbioni kukamilika
Wizata ya Viwanda yapongezezwa kasi mageuzi kiuchumi