May 14, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamishna Kuji awaapisha Makamishna wapya wa Uhifadhi TANAPA

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KAMISHNA wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Musa Nassoro Kuji Mei, 12, 2025 amewaapisha na kuwavisha vyeo Makamishna Wasaidizi wa Uhifadhi Tisa (9) ili kuboresha utendaji kazi wa Shirika hilo.

Zoezi hilo limefanyika katika Ofisi za TANAPA Makao Makuu jijini, Arusha.

Akizungumza katika hafla hiyo Kamishna Kuji, ametoa msisitizo kwa Makamishna hao kufanya Kazi kwa bidii, weledi na kusikiliza watu wanaowaongoza ili kuleta tija zaidi pamoja na kufikia malengo ya Shirika na Taifa kwa ujumla.

“Nendeni mkachape kazi kwa bidii na weledi huku mkiishi viapo vyenu mlivyoapa leo. Kiongozi mzuri ni yule anaesikiliza mawazo ya watu wake anaowaongoza hivyo, mkasikilize watu mnaowaongoza,” amesisitiza Kamishna Kuji.

Akitoa shukurani kwa niaba ya Makamisha wapya, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Simon Aweda ambaye ndiye Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Burigi-Chato alishukuru Bodi ya Wadhamini TANAPA pamoja na Uongozi wa Shirika kwa kutambua juhudi zao na kuamua kuwapandisha vyeo.

“Napenda kuchukua nafasi hii kwa niaba ya Makamishna wenzangu wapya kuishukuru Bodi ya Wadhamini na Uongozi wa Shirika kwa kutuamini na kutukabidhi majukumu haya kama tulivyotoka kuapa.

“Tunaahidi kufanya kazi kwa bidii na weledi wa hali ya juu ili kufanikisha malengo ya Taasisi ya kuendeleza Uhifadhi endelevu na kukuza Utalii katika Hifadhi za Taifa,” amesema Kamishna Aweda.

Makamishna wa Uhifadhi Wasaidizi walioapishwa ni pamoja na Simon Aweda, Catherine Mbena, Marckyfarreny Rwezaula, Nuhu Masay, Glads Ng’umbi, Dkt. Halima Kiwango, Halid Mngofi, Catherine Mwamage, na Julius Rutainurwa.