May 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waliopata ufaulu wa juu kidato Cha sita mchepuo wa sayansi kupata ufadhili

Na Joyce Kasiki, Dodoma

WIZARA  ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewasilisha ombi la bajeti ya Shilingi trilioni 2.4kwa mwaka wa fedha 2025/2026, kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake mbalimbali ambapo kwa mara ya kwanza, Serikali imetangaza mpango wa kutoa ufadhili kwa wanafunzi waliofaulu kwa kiwango cha juu katika kidato cha sita kwenye mchepuo wa Sayansi .

Mpango huo utawawezesha wanafunzi hao  kujiunga na shahada ya kwanza katika vyuo vikuu mashuhuri duniani na kwamba ufadhili huo utawalenga kusomea taaluma za kisasa kama Data Science, Artificial Intelligence (AI), Machine Learning (ML) na taaluma nyingine zinazohusiana.

Akizungumza Bungeni jijini Dodoma Leo Mei 12,2025 wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema mpango huo utajulikana kama Mama Samia Scholarship Extended for Data Science, Artificial Intelligence (AI) and Allied Sciences (Mama Samia 360 – DSP/AI+).

Amesema lengo kuu la mpango huo ni kuzalisha wataalamu wabobezi katika Data Science ili waweze kufanya kazi na kushindana katika soko la kimataifa.

Mkakati wa utekelezaji wa programu hiyo umegawanyika katika ngazi tatu ambazo ni kuwajengea uwezo vijana waliomaliza kidato cha sita kupitia kambi maalum kwa muda wa miezi 10 na kwamba mafunzo hayo yatatolewa na wataalamu kutoka sekta binafsi pamoja na wataalamu wazawa wanaoishi nje ya nchi (diaspora). 

Amesema mafunzo hayo yatahusisha msingi wa matumizi ya kompyuta, programu na uchambuzi wa mifumo,ujuzi laini kama uongozi na lugha,uzalendo,utamaduni wa nchi watakazokwenda kusoma.

Kwa mujibu wa Prof Mkenda Washiriki watapewa cheti cha ushiriki chenye hadhi ya kimataifa huku akisema,programu hiyo itawawezesha kupata udahili na ufadhili katika vyuo mbalimbali duniani.

Aidha amesema vijana waliomaliza shahada ya kwanza pia watapewa nafasi ya kuongeza ubobezi katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela na Indian Institute of Science and Technology – Kampasi ya Zanzibar.

Kwa upande mwingine amesema  Serikali itaendelea kufadhili wanafunzi wenye ufaulu wa juu katika masomo ya Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia kupitia SAMIA Extended Scholarship, kwa ajili ya kujiunga na shahada za juu.