May 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU Kagera yaokoa zaidi ya milioni 52.6

Na Ashura Jumapili TimesMajira online ,Bukoba,

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Kagera imeokoa zaidi ya milioni 52.6 kwa kipindi cha miezi mitatu,fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Missenyi pamoja na fedha za wananchi 9 waliotapeliwa kuunganishiwa umeme.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mjini Bukoba,Kaimu Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Kagera,Hajinas Onesphory,amesema kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu,wamefanikiwa kurejesha vigae vyenye thamani ya zaidi ya milioni 50,kutoka kwa mzabuni aliyepewa kazi ya kujenga hospitali ya Wilaya ya Missenyi.

“Katika ufuatiliaji tulibaini vigae hivyo, vilivyonunuliwa na Serikali havikuwasilishwa kwenye mradi huku nyaraka zote za mapokezi na manunuzi zikionesha kuwepo na kupokelewa kwenye mradi,”amesema Onesphory

Amesema baada ya kubaini hilo,walimshirikisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Missenyi,ambapo vigae hivyo vinarejeshwa na kuendelea na ujenzi wa hospitali hiyo huku hatua dhidi ya mtuhumiwa zitachukuliwa pindi uchunguzi utakapokamilika.

Sanjari na hayo, amesema kupitia dawati la uchunguzi la TAKUKURU,wamefanikiwa kusaidia wananchi tisa wa kijiji cha Bulembo kata Ibuga wilayani Muleba, waliokuwa wamedhulumiwa kiasi cha milioni 2.3, fedha walizochangishwa kwa ajili ya kuunganishiwa umeme kupitia mradi wa wyakala wa Umeme vijtijini (REA) unaotekekezwa na kampuni ya Nakuroi Investment Ltd wilayani humo.

“Kijiji hicho hakikiwemo katika mpango wa kufikishiwa umeme kwa wakati huo,hivyo mafundi hao waliwalaghai wananchi watoe fedha hizo ili wapelekewe umeme huku wakijua wazi kuwa jambo hilo haliwezekani,baada ya kupata taatifa hiyo tulifanya uchunguzi na kuwafikisha mahakama watuhumiwa wawili,”ameeleza Onesphory

Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Patric Method na Revocatus Masanja ambapo walifikishwa katika mahakama ya wilaya ya Muleba kwa makosa ya rushwa chini ya kifungu cha 15 cha kupambana na rushwa, ambapo baada ya kesi hiyo kusikilizwa mbele ya Hakimu Daniel Nyamkyelya walitiwa hatiani kwa makosa ya udanganyifu na mahakama iliwaamuru fedha zote milioni 2.3 zirejeshwe.

Fedha hizi zimekabidhiwa kwa wananchi hao tisa na taasisi hiyo na watuhumiwa wamechukuliwa hatua ya kufukuzwa kazi na mwajiri wao ambaye ni kampuni ya Nakuroi.

Mmoja wa wananchi waliorejeshewa fedha zao Akwilina Philemoni, amesema kupitia TAKUKURU,wameweza kurejeshewa fedha zao.