IDADI ya watu wenye ulemavu nchini Tanzania imeongezeka hadi kufikia watu milioni 5.3 sawa na asilimia 11.2 ya watanzania wote,kwa mujibu wa sensa ya watu na Makazi ya 2022 ikilinganishwa na asilimia 9.5 ya 2012 jambo linaloonesha uhitaji mkubwa wa kuboresha huduma,sera na miundombinu rafiki kwa kundi hili muhimu katika jami
Akizungumza Mei 9,2025 katika kongamano la Watu wenye Ulemavu lililoandaliwa na Ikupa Trust Fund ambapo pamoja na mambo mengine, watu wa kundi hjilo walijengewa uelewa juu ya mfumo wa kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST)) Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete, amesema idadi hiyo inaonesha jitihada kubwa zinahitajika katika kushughulikia masuala ya watu wa kundi hilo.
Aidha amesema, Serikali imejipanga kuendelea kuwawezesha watu wenye ulemavu na kuhakikisha wanajumuishwa kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
Amesema Serikali imeendelea kuboresha miundombinu rafiki katika sekta ya afya, elimu na huduma nyingine muhimu. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, Wizara ya Afya imetenga fedha mahsusi kwa ajili ya watu wenye ualbino, ikiwemo ruzuku ya upatikanaji wa mafuta maalum katika vituo vya afya.
Mbunge wa Viti Maalum na Mkurugenzi wa Ikupa Trust, Mhe. Stellah Ikupa, ameomba mfuko wa watu wenye ulemavu utenganishwe na mifuko mingine ili utekeleze majukumu yake kwa ufanisi, hasa katika maeneo ya afya, elimu na ustawi wa jamii. Pia ametangaza kuwa watu wenye ulemavu wametoa mchango wa shilingi milioni moja kusaidia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuchukua fomu ya kugombea urais mwaka 2025, wakitambua mchango wake mkubwa kwa kundi hilo.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju, amewasihi watu wenye ulemavu kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la wapiga kura, kushiriki chaguzi na kugombea nafasi mbalimbali ili waweze kuwakilishwa ipasavyo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA), Winfrida Samba amehimiza watu wenye ulemavu kutumia mfumo wa upendeleo katika zabuni za serikali ili kujiongezea fursa za kiuchumi.
Watu wenye ulemavu wameishukuru Serikali kwa kuboresha Sera ya Watu Wenye Ulemavu, wakisema ilikuwa ni kilio cha muda mrefu. Pia wamepongeza jitihada za kuwawezesha kupitia mikopo na ajira, ambazo zimewasaidia kujitegemea.
Hata hivyo, wameitaka Serikali kuhakikisha utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote unazingatia hali ya watu wenye ulemavu, wengi wao wakiwa hawana uwezo wa kugharamia matibabu. Pia wameomba dawa za magonjwa ya akili na mafuta ya watu wenye ualbino zipatikane bure katika vituo vya afya kama ilivyokusudiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Jabir Shekimweri, ameahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na watu wenye ulemavu katika kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
More Stories
TAKUKURU Kagera yaokoa zaidi ya milioni 52.6
Na Israel Mwaisaka,Rukwa
Madiwani Ilala walia na dampo la Pugu