May 2, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Biteko,atoa agizo kwa TPDC kuongeza kasi uendelezaji vitalu

📌 Asema lengo ni kuendelea kuwa na uhakika wa usalama wa nishati nchini

📌 Azindua mkakati wa kwanza wa muda mrefu wa TPDC (2025-2050)

📌 Asisitiza jamii zinazozunguka miradi ya mafuta na gesi asilia kutopuuzw

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko,ameliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuongeza kasi ya uendelezaji wa vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia ikiwemo Mnazi Bay Kaskazini, Eyasi Wembere, Songo Songo Magharibi.

Pamoja na mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia (LNG) ili nchi iendelee kuwa na uhakika wa upatikanaji wa nishati kwa ajili ya soko la ndani na nje.

Dkt.Biteko,ametoa agizo hilo jijini,Dodoma wakati akizindua mkakati wa muda mrefu wa TPDC) wa miaka 25 wa 2024/25 hadi 2049/50, ambao umeweka mipango na malengo ya kuleta uhakika wa upatikanaji wa nishati nchini.Mkakati ambao utaisaidia nchi kutumia kikamilifu rasilimali za mafuta na gesi zilizopo katika maeneo mbalimbali.

”Tunapozindua mpango huu wa miaka 25, ni muhimu tutambue kuwa jukumu muhimu la TPDC ni kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa nishati nchini.Tukumbuke kuwa sekta ndogo ya mafuta na gesi ina mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa hili,”amesema Dkt. Biteko.

Pia ameiagiza TPDC, kuimarisha mtandao wa mabomba na mifumo ya usambazaji wa gesi nchini kupitia teknolojia za Mini-LNG na CNG ili kuwafikia wananchi wengi ambao wapo mbali na bomba la usafirishaji wa gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar-es-Salaam.

Pamoja na kujiimarisha kifedha ili kuweza kutekeleza miradi mbalimbali kwa kubuni mifumo ya ubunifu ya utekelezaji wa miradi, kuboresha shughuli za kibiashara na kuendelea kupunguza utegemezi kwa ufadhili wa Serikali.

Vilevile ameitaka TPDC kudumisha uwazi, uwajibikaji na kuzingatia kanuni za mazingira, jamii na utawala (ESG),pamoja na kufanya kazi kwa karibu na kampuni za kimataifa za nishati, wawekezaji binafsi na wadau wa maendeleo ili kuvutia mtaji, utaalamu, na teknolojia inayohitajika kwa mafanikio ya mpango uliozinduliwa.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameendelea kusisitiza kuhusu miradi ya mafuta na gesi Asilia kutopuuza jamii zinazozunguka miradi hiyo kwani jamii hizo zinapaswa kuona manufaa ya rasilimali zilizopo katika maeneo hayo na wao wakiwa ndio walinzi wakuu wa miradi hiyo ambayo ni muhimu kwa uchumi.

Vilevile ameiagiza TPDC kuhakikisha wanalipa kipaumbele suala la nishati safi ya kupikia kwa kuendelea kusambaza gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya kupikia na hivyo kupunguza hewa ukaa na uchafuzi wa mazingira kutokana na matumizi ya mkaa na kuni.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa Serikali ya Mapiduzi Zanzibar, Shaib Kaduara,ameeleza kuwa mkakati huo unatoa mwanga wa kukua kwa uchumi wa watanzania na kielelezo cha mafanikio katika sekta ya nishati,huku akisisitiza kuwa amani na umoja ndiyo msingi wa maendeleo.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema kuwa, kuzinduliwa kwa mpngo huo kunaonesha jinsi nchi inavyopiga hatua kwa maendeleo.

Amesema Mkoa wa Dodoma upo tayari kupokea miradi ya gesi asilia kwa ajili matumizi mbalimbali ikiwemo kupikia na kuendesha vyombo vya moto kama magari.

Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Balozi Ombeni Sefue,amesema kuwa mpango huo unaenda sambamba na Ilani ya Chama cha Mapinduzi kuhusu masuala ya nishati.

Pia unalingana kwa karibu na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, hasa katika maeneo ya kuimarisha sekta ya nishati kama kichocheo kikuu cha uchumi wa viwanda, maendeleo ya miundombinu, kukuza matumizi ya teknolojia bunifu, kuongeza ajira na mapato ya Serikali, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika, safi na nafuu kwa Watanzania wote.

Ameeleza kuwa, kupitia mpango huo, TPDC inakusudia kuongeza matumizi ya gesi asilia nchini kutoka matumizi ya kawaida kama uzalishaji wa umeme, viwandani, kupikia nyumbani na nishati mbadala kwa magari kwenda kwenye matumizi ya kuongeza thamani kama vile kutumia gesi asilia kama malighafi katika viwanda vya petrokemikali, ikiwemo uanzishaji wa kiwanda cha mbolea.