May 2, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yasisitiza utamaduni wa kujikinga mahali pa kazi

Na Bakari Lulela, Timesmajira Online Singida

SERIKALI imetoa wito kwa waajiri, wafanyakazi na wananchi,kujenga utamaduni wa kujikinga dhidi ya ajali na magonjwa mahali pa kazi,ili kuepuka athari zinazoweza kutokea katika uchumi na ustawi wa wafanyakazi nchini.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete,katika maadhimisho ya siku ya usalama na afya mahali pa kazi duniani,kitaifa yamefanyika mkoani Singida.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo inasema,”Nafasi ya Akili Mnemba na Teknolojia za kidijitali katika kuimarisha Usalama na Afya Mahali pa kazi”.

Kikwete amesema, Serikali inatambua umuhimu wa kulinda nguvu kazi yake,hivyo imeendelea kuiwezesha Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa kazi (OSHA) kutekeleza wajibu wake kikamilifu.

“Serikali imechukua hatua mahsusi kuimarisha usalama wa wafanyakazi katika miradi ya kimkakati ikiwemo reli ya kisasa (SGR),barabara za mwendokasi jijini Dar-es-Salaam,bwawa la Mwl.Nyerere na mingine mingi, kwa kuhakikisha uwepo wa Maofisa usalama na afya,kwa ajili ya kutoa mafunzo ya mara kwa mara pamoja na kuwapatia vifaa kinga,”.

Amesema Serikali imeanza kuchukua hatua kuandaa sera zinazo wajumuisha wajasiriamali wadogo katika fursa mbalimbali kiuchumi, yakiwemo masuala ya usalama na afya kazini.

Ambapo OSHA, imeanzisha programu maalumu ijulikanayo Afya Yangu-Mtaji Wangu, inayowezesha kutambua makundi ya wajasiriamali wadogo na kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa kuzingatia kanuni bora za usalama na afya kazini.

Sanjari na hayo Kikwete,amesema teknolojia ina michango mkubwa katika kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, ambapo amewashauri waajiri kujiweka tayari kupokea mabadiliko ya teknolojia huku wakichukua tahadhari dhidi ya athari hasi za teknolojia ikiwemo kuhatarisha baadhi ya fursa za ajira kupotea.

Awali Mtendaji Mkuu wa OSHA,Khadija Mweda, amesema maadhimisho yanalenga kuhamasisha uzingatiaji wa kanuni bora za usalama na afya mahali pa kazi nchini.Ambapo Taasisi yake uratibu maadhimisho hayo kwa niaba ya Serikali kwa kushirikiana na wadau ambao ni Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA),Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na Shirika la Kazi Du

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ATE,Suzanne Ndomba-Doran,ameshauri matumizi ya teknolojia mbalimbali ikiwemo akili unde ili kuongeza ufanisi katika uzalishaji.

Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya, ametoa tahadhari kwa waajiri nchini,kuhakikisha teknolojia mpya zinatumika katika uzalishaji na haziathiri ajira za Watanzania.