November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadada Solutions kuendelea kupinga ukatili

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

SHIRIKA la Wadada Solutions on Gender Based Violence limesema litaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali na wadau mbalimbali za kupambana na ukatili pamoja na kuwekeza kwenye afya ili kuhakikisha jamii na watoto wa kike wanakuwa salama.

Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Mradi Haki ya Binti awamu ya pili wa Shirika la Wadada Solutions on Gender Based Violence, Karus Masinde
wakati wakikabidhi msaada wa vifaa vya kunawia mikono kwa ajili ya kujikinga na maradhi mbalimbali ikiwemo Corona na kudai kupitia mradi huo wataendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kupambana na ukatili na magonjwa mengine ya mlipuko ili kuwe na Taifa salama.

Matenki na vifaa hivyo vya kusafishia mikono vimetolewa katika shule za Sekondari Mihama na Kitangiri ambapo mradi huo unatekelezwa ili wanafunzi waweze kujikinga na magonjwa yanayosababishwa na uchafu na kuimarisha afya zao.

“Leo tumekuja kutembelea shule ya Sekondari Mihama na Kitangiri na kuwaletea matenki kwa ajili ya kuwekea maji,sabuni na vitakasa mikono kwa ajili ya kusafishia mikono ili kujikinga na magonjwa mbalimbali ikiwemo ya homa kali ya mapafu unaosababishwa na kirusi aina ya Corona (COVID-19),”.

“Pia tunaendelea kupinga ukatili kama tunavyoona kipindi cha likizo watoto wamekuwa nyumbani na kesi nyingi za mimba kutokana na Corona zimeongezeka,na sisi kama wadau tunaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuweza kupambana na magonjwa mbalimbali pia kuhakikisha mtoto wa kike anakuwa salama na kuepukana na mimba za mapema,”amesema Masinde.

Ofisa Mradi wa Haki ya Binti awamu ya pili wa Shirika la Wadada Solutions on Gender Based Violence, Karus Masinde (kushoto) akishikana mkono na mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kitangiri baada ya kukabidhi tenki na vifaa vya kunawia mikono kwa ajili ya kujikinga na kuimarisha usafi shuleni hapo. (Picha na Judith Ferdinand).

Makamu Mkuu wa shule ya Sekondari Mihama, Francis Ouma amelishukuru Shirika hilo kwa kuwapatia vifaa hivyo vya kujikinga na magonjwa ya kuambukizwa vinawafaa kutokana na hali halisi hapo shuleni ambao wanatumia ndoo za lita 20 ambazo zimewekwa kila darasa na ukilinganisha na idadi ya wanafunzi ambao 529 kidogo ilikuwa ni changamoto.

“Tenki hili la kuwekea maji litatusaidia kwa kiasi kikubwa sana, shirika limekuwa marafiki wazuri kwetu kwani wameanza kuwalea wanafunzi wetu tangu 2016 kwenye mradi wa Haki ya Binti awamu ya kwanza mpaka leo awamu ya pili wameendelea kuwalea pia ni washauri wazuri wa watoto wetu, kiasi imepelekea tuwe na watoto wazuri ambao wanapendeza kwenye jamii ambapo kupitia shirika hilo mimba zimepungua na katika kipindi cha corona hawajapokea kesi ya mimba,” amesema Mwalimu Ouma.

Kwa upande wake, Dada Mkuu wa shule ya Sekondari Mihama, Rahma Suleimani amesema, tenki hilo litawasaidia katika utunzaji wa maji kwani yalipokuwa yakikatika wanakosa maji ya ziada na kuliomba Shirika hilo kuendelea kuwasaidia kwani changamoto ni nyingi shuleni hapo ikiwemo kukosekana kwa taulo za kike na kuwa na chumba kidogo cha kujihifadhia wakati wa hedhi na matundu ya vyoo vya watoto wa kike ni machache ambayo yapo 6 ukilinganisha na idadi yao ambao wapo zaidi ya 200.

Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi wa Shule hiyo, Charles Robert amesema, vifaa hivyo vitasaidia kuhifadhi maji ambayo yatakuwa ni msaada kwao kwa kuhakikisha suala la usafi la unawaji mikono linazingatiwa na ikizingatiwa kipindi walichotoka hapo nyuma kulikuwa na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na kirusi cha Corona na bado tahadahari inaendelea kuchukuliwa.

Amesema tangu wametoka kwenye likizo ya corona walimu wao wanejidhatiti kuwaelimisha namna ya kujikinga na ugonjwa huo kwa kunawa mikono na kuvaa barakoa ingawa suala la kuvaa barakoa halikutiliwa maanani ila la kunawa mikono hadi leo linaendelezwa.

Mlezi wa klabu ya Wadada Centre shule ya Sekondari Kitangiri, Mwalimu Nezia James amesema, vifaa hivyo walivyopatiwa na shirika hilo vitawasaidia katika masuala ya usafi na shule yao ni ya kutwa hivyo muingiliano ni mkubwa itasaidia kuboresha afya zao,na kupitia miradi ya haki ya Binti imesaidia mabinti kujitambua,kujikomboa na ukatili wawapo nyumbani na njiani pamoja na mimba zimeweza kupungua huku baada ya kufungua shule bado hawajapata kesi yoyote ya mimba.