Na Bakari Lulela, TimesMajira Online
MKUU wa Wilaya ya Moshi, Mwangi Kundya amewataka waajiri Mkoani Kilimanjaro kuwekeza kwenye masuala ya usalama na afya kwa wafanyakazi.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro kwenye uzinduzi wa mkakati wa kupunguza ajali na magonjwa sehemu za kazi maarufu kama ‘Vision Zero’ mjini Moshi, Kundya amesema endapo waajiri watawekeza kwenye masuala ya Usalama na Afya kwa kuweka mikakati endelevu ya kuwalinda wafanyakazi wataweza kuongeza tija kwenye masuala ya usalama na uzalishaji utaongezeka jambo ambalo litakuza mapato na kuwa chachu katika ongezeko la kodi vitakavyopelekea kukuza uchumi wa Taifa.
Mkurugenzi wa Usalama na Afya Mhandisi Alex Ngata aliyemuwakilisha Mtendaji mkuu wa OSHA amesema, mafunzo hayo yameandaliwa mahususi kwa ajili ya kuwawezesha waajiri nchini kuhakikisha wanapunguza ama kuondosha kabisa ajali na magonjwa sehemu za kazi.
Amesema, mafunzo hayo ambayo tayari yamefanyika katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Arusha na sasa Kilimanjaro yatawasaidia waajiri kuweka mikakati madhubuti kwenye maeneo yao ya kazi, katika kupunguza au kuondosha ajali na magonjwa sehemu za kazi.
“Sambamba na mafunzo hayo, pia tunapata wasaha wa kusikiliza kero na changamoto zao, wakati wa utekelezaji wa sheria namba 5 ya mwaka 2003 ya usalama na afya na kuzitatua,” amesema Ngata.
Afisa mtendaji wa chama cha wafanyabiashara, viwanda na kilimo nchini (TCCIA) Mkoa wa Kilimanjaro, Boniface Mariki amesema, mafunzo hayo yatawasaidia sana katika utendaji kazi zao kwani wafanyakazi ni kiungo katika utekelezaji wa shughuli za viwanda endapo mfanyakazi ataumia itakuwa gharama kubwa kumtibia na vilevile shughuli za uzalishaji zitaathirika.
Mariki amesema, wanachama wake wamefurahi kupata mafunzo hayo kwani vision zero ni mpya kwao hivyo wanamuahidi kutekeleza ipasavyo mkakati huo ambao umelenga kupunguza ajali na magonjwa sehemu za kazi pamoja na kuiomba OSHA kuendelea kuwapatia mafunzo kama hayo.
Afisa mtendaji huyo wa (TCCIA) amesema endapo waajiri watatenga bajeti zao za utekelezaji wa masuala ya usalama na afya kazini zitasaidia sana kuendeleza mipango yao hivyo kuwa na uhakika wa uzalishaji.
Kwa upande wake mkurugenzi wa huduma za Tathmini toka mfuko wa fidia kwa wafanyakazi (WCF) Dkt. Abdulsalum Omari amesema waajiri wanapaswa kufanya tathmini ya hali hatarishi sehemu zao za kazi lakini pia kutengeneza shabaha ili kutambua kuna ajali kiasi gani ili waweze kuweka mifumo ya kudhibiti ajali na magonjwa sehemu za kazi.
Naye mkuu wa kitengo cha sheria kutoka OSHA, Joyce Mwambungu amesema, mwaka huu wa fedha 2020/2021 wakala wamelenga kujenga uelewa zaidi kwa wadau wao katika masuala mbalimbali ya usalama na afya ili kutatua changamoto wakati wa utekelezaji wa sheria ya usalama na afya mahala pakazi.
Amesema, yapo maboresho mengi ambayo OSHA imeyafanya na inaendelea kufanya ili kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji biashara kwa wadau na mpaka sasa Tozo na ada mbalimbali zilizokuwa zikitozwa zimeweza zimeondolewa ili kurahisisha utekelezaji wa sheria.
Akifafanua kuhusiana na tozo, amesema kwa mwaka huu wa fedha kupitia bajeti iliyosomwa na waziri wa fedha wameondoa tozo ya Elimu kwa Umma ambayo ilikuwa ikitozwa hivyo ni fursa kwa waajiri kuwasiliana na OSHA kwa kumuandikia mtendaji mkuu.
“Tozo za mafunzo zipo kisheria zinabaki kama ilivyo lakini tozo ya elimu kwa umma ndio imefutwa hivyo waajiri watapatiwa elimu hiyo bure ambayo ilikuwa ikitozwa endapo OSHA itakuja kukupatia elimu,” ameongeza Mwambungu
Mafunzo ya vision zero mkoani Kilimanjaro yameandaliwa na OSHA kwa kushirikiana na TCCIA mkoani Kilimanjaro kwa lengo la kuwatambulisha vision zero kwa waajiri na wanachama wa TCCIA mkoani Kilimanjaro.
More Stories
Balozi Nchimbi kuongoza waombolezaji mazishi ya Kibiti leo
Dkt.Tulia,apewa tano kuwezesha wananchi
Nkasi yajipanga kukusanya mapatoÂ