Na WMJJWM- Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewafuturisha Watoto wanaolelewa katika Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo Dodoma katika Kipindi hiki cha mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Akizungumza wakati wa Iftari hiyo kwa niaba yake, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis alitoa shukurani kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi yenye lengo la kuondoa kabisa changamoto zinazowakabili watoto walio katika mazingira hatarishi.
“Kipekee kabisa, ninamshukuru tena Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kufuturisha watoto wanaoishi katika Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo pamoja na maeneo mengine ya nchi hususani Watoto wa Mkoa wa Arusha na Dar Es Salaam”. ameeleza Naibu Waziri Mwanaidi.
Aidha aliongeza kuwa Wizara inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na wadau kwa lengo la kuhakikisha watoto walio katika mazingira hatarishi wanapatiwa huduma ya malezi ya muda mfupi katika Makao ya Watoto.
“Serikali na Wadau tutaendelea kushirikiana kutoa huduma kulingana na sheria, kanuni na miongozo tuliyojiwekea, nitumie fursa hii kuwaomba wamiliki wa makao ya kulelea watoto kuhakikisha mnatoa huduma kwa mtoto kwa kuzingatia maslahi mapana ya mtoto”. amesema Naibu Waziri Mwanaidi.
Mhe. Mwanaidi alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi, walezi na watendaji wa Wizara kwa kuendelea kuratibu na kusimamia utekelezaji wa afua za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto katika makao yote hapa nchini.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt.John Jingu amewasihi watoto waishio katika makao hayo kuishi kwa upendo na amani huku wakiweka bidii katika masomo yao na stadi za kazi kwa ujumla ili waweze kufikia malengo yao ya baadae.
Naye Mwakilishi kutoka Shirika la Abbot fund Edna Hauli ameipongeza Serikali kwa juhudi zake katika kuhakiksha watoto wanakuwa salama na kuahidi kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha watoto wanapata mahitaji yao muhimu na kuweza kufikia utimilifu wao kama binadamu.
Sanjari na hilo katika tukio hilo pia kuliambatana na tukio la kukabidhi mashine ya kufulia 4, printer na photocopy mashine 1, vitabu 1670 friji 2 nguo na mahitaji mengine ambavyo vilitolewa na Shirika la Abbot Fund vikiwa na thamani ya shiling Milioni 88 ili viweze kurahisisha majukumu ya utendaji kazi ndani ya Makao hayo.
More Stories
The Desk and Chair yatoa vifaa saidizi kwa Masatu na mkewe
jengo la mama,mtoto la bilioni 6.5 lazinduliwa Mbulu
Dkt.Malasusa ataka hospitali ya Haydom kuombea wafadhili wanaoishika mkono