*Zaidi ya Shilingi Bilioni 21 zatumika kulipa fidia waliopisha mradi
*Serikali yasema mradi utakamilika kwa wakati
Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa Umeme wa Tanzania na Zambia (TAZA), unaohusisha njia ya kusafirisha umeme wa Msongo wa Kilovolti 400 pamoja na Vituo 5 vya kupoza umeme kikiwamo kituo cha Kisada. Hata hivyo Kamati hiyo imeeleza kuridhishwa kwake na hatua ya utekelezaji wa mradi huo.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, David Mathayo amesema hayo wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme katika Mkoa wa Iringa tarehe 19 Machi 2025 ukiwemo mradi wa TAZA.

Mathayo amesema, Mradi huo ni muhimu kwa kuwa una manufaa makubwa kwa nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika ambapo utawezesha nchi hizo kuuziana umeme kupitia Tanzania.
Ameeleza kuwa, mradi huo utakapokamilika utaimarisha hali ya upatikanaji wa umeme katika Mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Songwe pamoja na kufikisha umeme wa Gridi katika Mkoa wa Rukwa.

Aidha, amesema kukamilika kwa mradi huo kutawezesha ujenzi wa njia ya kusafirisha Umeme wenye msongo wa Kilovolti 400, kutoka Sumbawanga kupitia Mpanda na ujenzi wa Kituo cha kupoza umeme katika eneo la Kidahwe mkoani Kigoma hali itakayoimarisha umeme katika Mkoa wa Rukwa, Katavi, Kigoma na Tabora.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko amesema tayari Serikali imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 21 kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi waliopisha eneo la ujenzi wa mradi pamoja vituo vya kupoza umeme.

Kapinga amesema, tayari zaidi ya shilingi Bilioni 17 zimeshalipwa kwa Wananchi zaidi ya elfu 6 ambao maeneo yao yamechukuliwa kwa ajili ya kupisha ujenzi wa Mradi huo.
Amefafanua kuwa, mradi huo unajengwa kwa fedha za Watanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB), Shirika la Maendeleo la Ufaransa(AFD) na Umoja wa Ulaya(EU).
Akizungumzia ujenzi wa Kituo cha Kisada, Kapinga amesema zaidi ya wakazi 70 wanaozunguka eneo hilo watapata ajira za muda mfupi, huduma ya maji safi na salama pamoja na kuboreshewa Barabara ya kutoka Nyororo kwenda Kisada yenye urefu wa kilomita 15 kutoka Barabara kuu iendayo Mbeya.
Amesema, Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa mradi huo muhimu ili ukamilike kwa wakati na kuleta matokeo Chanya yaliyokusudiwa ikiwemo upatikanaji wa umeme wa uhakika na wakutosha kulingana na mahitaji ya nchi.


More Stories
NACTVET yawahakikishia wadau, usimamizi thabiti wa ubora wa elimu ya Ufundi na Amali
Wasira awataka Wenyeviti CCM kuiga mfano Mkoa wa Mbeya
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,yajizatiti kuboresha uwezo wa Mawakili wa Serikali