Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online
KAMISHNA wa Uhifadhi Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Musa Nassoro Kuji, amehimiza maafisa na askari wa Hifadhi ya Taifa Burigi – Chato kuwajibika kikamilifu katika kuboresha na kuimarisha shughuli za uhifadhi na utalii.
Kamishna Kuji ameyasema hayo leo Machi 16, 2025, alipofanya ziara ya kikazi katika hifadhi hiyo kwa lengo la kukagua shughuli za uhifadhi na utalii.
Katika ziara hiyo alipokelewa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Izumbe Mgana Msindai – Kamanda wa Uhifadhi wa Kanda ya Magharibi na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Simon Aweda – Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Burigi-Chato.

“Ongezeni ubunifu katika utendaji kazi ili kuboresha na kuimarisha shughuli za uhifadhi na utalii na kuongeza idadi ya watalii na mapato kufikia azma ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya kufikisha idadi ya watalii milioni 5 na mapato ya dola bilioni 6 za Kimarekani kwa mwaka wa fedha 2025,” amesema Kamishna Kuji.
Aidha, amesisitiza matumizi mazuri ya rasilimali watu pamoja na kuruhusu ubunifu wenye tija ili kuleta matokeo chanya.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Simon Aweda alimshukuru Kamishna Kuji kwa kutenga muda wake na kukutana na watumishi.
Ameeleza kuwa, hifadhi inaendelea na mikakati ya kuboresha miundombinu ya utalii na kuimarisha shughuli za ulinzi na usalama, ikizingatiwa kuwa hifadhi hiyo ipo mpakani mwa nchi za Rwanda, Burundi na Uganda.

“Hifadhi yetu inazidi kuimarika kiusalama na ina nafasi kubwa ya kukua kiutalii kwani kuna fursa mbalimbali za uwekezaji wa kambi za watalii na hoteli.
“Tunaendelea kutangaza fursa hizi ili kuongeza mapato ya serikali na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa,” ameongeza Kamishna Aweda.
Hifadhi ya Taifa Burigi – Chato, iliyopo Kanda ya Magharibi, ni maarufu kwa wanyama adimu aina ya Mbega Wekundu Ashy Red Colobus Monkey.

More Stories
Kasi mageuzi chanya sekta ya elimu Musoma Vijijini yashika kasi
Mradi wa kuimarisha huduma za dharura kwa majeruhi wa ajali za barabarani wazinduliwa
MSIGWA:Mfumo wa usajili waandishi wa habari kidijitali upo mbioni kukamilika