Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KAMISHNA wa Shirika la hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA, Musa Kuji amewataka Maafisa na Askari wa Uhifadhi katika Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Rubondo kufanya kazi kwa uadilifu, weledi, bidii, nidhamu na ushirikiano ili kuimarisha uhifadhi wa hifadhi hiyo.
Kamishna Kuji ameyasema hayo Machi 15, 2025, alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua shughuli mbalimbali na kufanya kikao na Maafisa na Askari katika Makao Makuu ya hifadhi hiyo Kageye, Mkoa wa Geita.
“Ninawapongeza kwa kazi nzuri. Tuongeze bidii, nidhamu na ushirikiano ili kuimarisha ulinzi wa maliasili za Taifa,” amesema Kamishna Kuji.

Aliongeza kuwa Shirika litaendelea kuboresha maslahi ya watumishi, ikiwemo haki ya kujiendeleza kielimu, kupata matibabu, kupandishwa vyeo kwa kuzingatia vigezo na kusikilizwa kwa haki.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Dkt. Iman Kikoti, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Rubondo, alimshukuru Kamishna Kuji kwa ziara hiyo na kueleza kuwa hali ya uhifadhi inaendelea vizuri, doria zinaimarika, na idadi ya watalii imeongezeka hadi 2,076 kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Askari Uhifadhi Daraja la Kwanza Hiza Joseph Mahanyu alieleza furaha yake kwa ujio wa Kamishna Kuji, akisema ni ishara ya kuthamini mchango wa watumishi katika kulinda maliasili.
Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Rubondo, mojawapo ya hifadhi za Kanda ya Magharibi, inasifika kwa wanyama adimu kama sokwe, utalii wa matembezi ya miguu na boti, mchezo wa kuvua na kuachia samaki, safari za gari, na zoezi la kuzoesha sokwe (Chimpanzee Habituation Experience).
Pia ni kivutio kikubwa cha utalii katika ukanda wa Ziwa Viktoria, ikiwa na msitu mkubwa wa asili ya Congo (Low Congolese Forest).

More Stories
Kongani ya Viwanda ya Sino _Tan kutoa ajira laki moja
Waandishi wa habari kutambulika kidijitali
Mahundi awataka wanachuo kutoendekeza anasa