March 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NMB yafuturisha viongozi ALAT,wananchi

Na Joyce Kasiki,Dodoma

BENKI ya NMB imeandaa na kushiriki futari na Viongozi wa Jumuiya ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (ALAT) pamoja na baadhi ya wananchi wa mkoa wa Dodoma kwa lengo la kuendeleza kudumisha mshikamano na ushirikiano katika utendaji kazi miongoni mwao.

Akizungumza katika hafla hiyo,Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ameishukuru Benki hiyo na Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) kwa mchango wao katika kuendeleza maendeleo ya mkoa huo.

Aidha aliipongeza Benki ya NMB kwa kuendelea kiwahufunia wananchi lakini kwa jambo jema la kuandaa Ifutari ambayo kwa namna moja ama nyingine inajenga mahusiano mema baina ya viongozi ,wananchi na NMB.

Kwa upande wake, Afisa wa Wateja Wakubwa na Serikali wa Benki ya NMB, Alfredy Shayo, amesema hadi mwishoni mwa mwaka 2024, benki hiyo imefanikiwa kufikia vijiji 1,000 kupitia kampeni ya NMB Kijiji Day. Kampeni hiyo inalenga kuunga mkono jitihada za serikali za kuhakikisha kila Mtanzania, popote alipo, anapata huduma za kifedha, hatua inayochochea ukuaji wa uchumi wa taifa na mtu mmoja mmoja.

Shayo ameongeza kuwa kwa mwaka 2025, NMB inapanga kufikia wananchi 2,000 ili kuwawezesha kufungua akaunti ya NMB Pesa kwa gharama nafuu ya shilingi 1,000 pekee Akaunti hiyo inawapa wateja fursa ya kupata mikopo bila kulazimika kufika katika matawi ya benki.

Aidha amesema Benki ya NMB inatamani kutumia mwezi huu mtukufu wa Ramadhani kuombea uchaguzi wa amani.

Ametoa wito kwa Jumuiya ya ALAT kushirikiana na NMB katika kutoa elimu ya kifedha kwa wananchi.

Kwa niaba ya wajumbe wa ALAT Mkoa wa Dodoma, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, White Zuberi, ameishukuru NMB kwa kuwaunganisha katika hafla ya Iftar, akisema hatua hiyo inaonesha umuhimu wa mshikamano na ushirikiano kati ya taasisi za kifedha na viongozi wa serikali za mitaa.

Zuberi amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewatia moyo kwa kutambua jitihada za baadhi ya halmashauri katika kuwahudumia wananchi kwa niaba ya Serikali Kuu.

Amesema kutambuliwa huko kunawapa nguvu zaidi ya kuendelea kuwatumikia wananchi kwa uadilifu.