Na Irene Mark,Timesmajira
MKURUGENZI wa Shirika la Marie Stopes Tanzania (MST), Patrick Kinemo amesema zaidi ya watanzania milioni mbili nchi nzima wamefikiwa na watoa huduma za Mkoba waliopo chini ya shirika lake kwa mwaka 2024.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, mbele ya wadau mbalimbali wa afya wakati wa madhimisho ya kuelekea siku ya Wanawake Duniani, Kinemo amesema kati ya waliofikiwa wanaume ni asilimia nne huku vijana wakiwa asilimia 20 tu.
Amesema idadi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 21 la watanzania waliofikiwa na huduma hizo kwa mwaka 2023/2024 huku akiahidi kuwafikia watanzania zaidi kupitia watoa huduma za Mkoba kwa mwaka 2025.
Aidha amewaomba waandishi wa habari kupeleka taarifa sahihi juu ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango kwa wanaume ili kuboresha uchumi wa familia na taifa.

“Baba wa familia akishiriki vizuri kwenye kupata ushauri na huduma kuhusu afya ya uzazi atamsaidia mama kuzuia mimba zisizotarajiwa na watapanga uzazi.
“Wenzetu nchi zilizoendelea zilianza kipanga uzazi mapema familia zikaweza kuwahudumia vizuri watoto wao na kuwapa ustawi unaotakiwa kwao,” alisema Kinemo akitolea mfano nchi za Bara la Asia.
Amesema idadi ya watanzania waliofikiwa kitaalam ikiwekwa kimahesabu ni sawa na kuzuia vifo 3430 vitokanavyo na uzazi kwa kipindi cha miaka mitano.

“Sisi MST tunashirikiana na serikali kuwajengea uwezo wa hudumu wa afya katika vituo 343 na mauguzi wao 43 ambao kwa pamoja wanasaidia wananchi kupata huduma bora za afya kwenye makazi yao.
Kwa upande wake Mkurungenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Afya, huduma za afya ya mtoto na Vijana, Idara ya Afya na Uzazi, Mama na Mtoto, Dk. Felix Bundala amesema serikali inajivunia kushirikiana na Marie Stopes kwani inasaidia kupunguza vifo na changamoto za uzazi.

“Kupitia huduma za Mkoba hawa wenzetu wanawafikia kwa karibu zaidi wananchi na kuwapa elimu ya magonjwa ya ngono na mimba, kinga yake na matibabu kwa makundi yote ya jamii zetu… Ni suala la kuwapongeza wadau hawa muhimu kwenye sekta ya afya hasa afya ya uzazi.
“Tuitumie siku ya wanawake duniani kujadili masuala ya afya kwa wote ili kuwahamasisha wanaume kuibeba ajenda ya afya ya uzazi kuwa sehemu yao, isiishie tu kumpeleka mwenza mjamzito kliniki,” amesema Dk. Bundala.
Dk. Gerald Kiwele ni Mratibu wa Kitaifa Masuala ya Afya ya Uzazi kwa Vijana na Jinsia kutoka Wizara ya Afya amesema jitihada kinaendelea kufanyika ili kuhakikisha ushiriki wa wanaume kwenye masuala ya afya ya uzazi unaongezeka.

Amesema suala la ushiriki wa wanaume lipo kwenye mpango wa afya hasa kwenye afya ya uzazi huku akisisitiza kwamba muongozo unatoa maelekezo ya namna mwanaume anavyoweza kumsaidia mwenza wake kuwa na afya bora na kwenye kushiriki uzalishaji mali huku wakihudumia familia yao na kuwa na kipato kizuri.
“Halafu uzazi wa mpango unaongeza upendo nyumbani wanaume wengi hawajui hii siri,” amesema Dk. Kiwele.
More Stories
Dkt.Samia atimiza ndoto ya wananchi Same,Korogwe,Mwanga ya kupata maji
Tanzania One yatoa msaada kwa wanawake hospitali ya Temeke.
Wanawake BUWASA watembelea wafungwa wanawake gereza la Bukoba