Na Mwandishi wetu, Timesmajira
Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kigamboni na Katibu wa Kamati ya Mapambano dhidi ya Ukatili kwa Wanawake na watoto UWT Taifa, Lilian Wasira amewaasa wanawake wavae kofia za ‘umeneja kampeni’ ili kuhakikisha Rais Samia Suluhu Hassan anapata kura za heshima kuliko ilivyowahi kutokea huko nyuma kutokana na namna alivyoliheshimisha Taifa na hususan wanawake.
Wasira amesema hayo kwa wanawake wajasiriamali wilaya ya Temeke wakati akizindua umoja wao ambapo amesema Rais Samia amekitendea haki kiti chake kwa kumwezesha mwananchi wa kipato cha chini hususan wanawake.
Amesema leo wanashuhudia serikali ikitoa mikopo bila riba na ya riba nafuu ili mwananchi wa kawaida aweze kuinuka kiuchumi.

“Hakuna kundi aliloacha Rais wetu, sio wasanii, sio wanamichezo, na ukiachana na mikopo ya halmashauri bado tuna mikopo nafuu sana ya WBN yani MACHINGA ambapo tayari bil 18 zimekwishawekwa benki ya NMB kwaajili yetu wajasiriamali, watu wameanza kupokea fedha, Mwenyezi Mungu atupe nini kinamama? Kama Rais tunaye, tutafute mengine,”amesema Wasira.

Wasira amesema Rais Dkt.Samia hajaishia hapo amekuwa kinara kusaidia wananchi wasiojiweza kupata msaada wa kisheria bure kabisa nchi nzima, ameeendeleza miradi mingi hivi sasa imekamilika, ameboresha sekta ya afya ameongeza zahanati, vituo vya afya na hospitali nchi nzima, ameinua sekta ya elimu nchini kwa kuongeza madarasa na ujenzi wa shule mpya na mabweni.
“Leo maeneo mengi watoto wetu wanasoma kwa kujidai kwasababu ya jitihada zake, hivyo kuwataka kinamama hao kujitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye daftari la wapigakura na pia kuhimiza wananchi wengine kufanya hivyo ili kipenga kikilia jambo liende sawia,”amesema
More Stories
STANBIC yaendelea kusaidia makampuni madogo ya uchimbaji mafuta na gesi
Mawakala kielelezo cha uwazi uboreshaji daftari la wapiga kura
Muhimbili:Tanzania ya kwanza kutumia mtambo unaotumia tiba hewa Afrika Mashariki na Kati