March 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nchi 28 Afrika zajadili mikakati kukabiliana na dawa,chanjo feki

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Dar-es-Salaam.

Nchi 28 zimekutana katika mkutano wa kimataifa wa Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH),Ukanda wa Afrika, lengo likiwa ni kujadili na kuweka mikakati ya kudhibiti madawa na chanjo feki kwa mifugo.

Miongoni mwa mikakati iliyopendekezwa ni kuanzisha mifumo madhubuti ya usajili na ufuatiliaji wa dawa zinazoingizwa na kutumika, hatua ambayo itasaidia kuziondoa dawa na chanjo zisizo na viwango stahiki sokoni.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mkutano huo uliofanyika Machi 4 mpaka 6, 2025 jijini Dar-es-Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, (Mifugo),Abdul Mhinte amesema Tanzania iko tayari kushiriki katika vita dhidi ya dawa na chanjo feki za mifugo.

Mhinte amesema,mkutano huo ni muhimu kwa Afrika, kwani kumekuwa na ongezeko la dawa na chanjo feki, jambo lililosababisha WOAH kuandaa mkakati maalum wa kusaidia nchi za Afrika na dunia kwa ujumla kupambana na tatizo hili.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi , Dkt. Benezeth Lutege, amesema Serikali imetenga bilioni 28.1 kwa ajili ya kampeni ya kitaifa ya chanjo kwa mifugo, ambayo itazinduliwa hivi karibuni.

“Chanjo zitakazotumika mwaka huu ni zile zinazozalishwa ndani ya nchi na kukaguliwa na mamlaka za Serikali, hatua ambayo itasaidia kuzuia uingizwaji wa chanjo na dawa feki zinazosababisha usugu wa magonjwa,” amesema Dkt. Lutege.

Amewataka wafugaji, waingizaji wa dawa na chanjo, pamoja na wazalishaji, kuzingatia kanuni na taratibu za uzalishaji, usambazaji, na uuzaji wa dawa hizo.

Naye Jane Royelo kutoka WOAH aliwahimiza wafugaji na wauzaji wa dawa za mifugo kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kuhamasishwa matumizi sahihi ya dawa na kuepuka matumizi mabaya ya dawa zisizohitajika.