Na Mwandishi Wetu, Pwani
OFISI ya Msajili wa Hazina pamoja na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeunda kamati ya pamoja ya kuangalia namna mashirika ya Umma yanavyoweza kujiendesha kwa faida na kuacha utegemezi wa Serikali.

Akizungumza na Waandishi wa habari jana Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu amesema kuwa makubaliano hayo yamefikiwa baada ya kikao kazi cha siku mbili kati ya Ofisi ya Hazina na Ofisi ya Taifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG.)kilichoketi katika chuo cha uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Mkoani Pwani.
Mchechu, alisema kuwa kamati hiyo ya pamoja ni sehemu ya utekelezaji wa R nne za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambazo kati ya hizo wamechukua mbili ikiwemo ya kusimamia mashirika kupunguza utegemezi na kufanya kazi kwa faida na kutoa gawio Serikalini.
Mchechu,amesema kuwa ofisi yake inasimamia taasisi 300 huku taasisi 250 zinasimamiwa na ofisi ya CAG na ndio maana wameona ni vyema kwasasa kufanyakazi kwa pamoja kwakuwa Ofisi ya CAG ni sehemu ya mafanikio yao.
Alisema kuwa,kikubwa kinachokwenda kufanywa ni kuongeza juhudi katika usimamizi bora wa rasilimali za Taifa ambapo ili kufikia mafanikio hayo tayari kwasasa wameweka mikakati ya pamoja ili kurahisisha usimamizi wa maeneo ya raslimali ya Taifa.
Katika kikao kazi hicho,ambacho kiliwashirikisha menejimenti ya Taifa ya Ukaguzi,menejiment ya ofisi ya msajili wa hazina pamoja na wataalam wa ofisi hizo Mchechu amesema wamekubaliana mambo mbalimbali ikiwemo kuangalia namna ya uboreshaji wa usimamizi wa taasisi za Umma pamoja na kusaidia katika vipaumbele vinavyotekelezeka na kuweka misingi yake.
Mchechu, aliongeza kuwa katika muendelezo wa hilo walilolifanya kuna taasisi tatu ambapo kwa ujumla wake ndio taasisi mtambuka huku akitaja taasisi hizo kuwa ni ofisi ya CAG,Wizara ya Fedha pamoja na ofisi ya Utumishi wa Umma.
Kwa upande wake Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali,(CAG).CPA Charles Kichere,amesema kuwa kikao kazi hicho cha siku mbili kilikuwa pia na lengo la kupata michango ya wadau kwa ajili ya kuboresha mashirika ya Umma.
Kichere,amesema kuwa kikao hicho pia kimempa fursa ya kujua changamoto na mapungufu katika mashirika ya Umma ambapo miongoni mwa changamoto alizobaini ni upungufu wa rasilimali katika mashirika hayo.
Kichere alisema kuwa mbali na hayo lakini mambo mengine yaliyofanyika katika kikao kazi hicho ni kufanya tathmini ya mbinu chanya ya namna ya kubadili mashirika hayo,ufanisi katika matumizi ya rasilimali, masuala ya teknolojia na ubunifu katika kuboresha huduma na mafunzo kwa watumishi Umma.
“Tumeona kuna umuhimu wa kukutana ili tuweze kufikia malengo ya taasisi kwa haraka na tunataka mashirika ya Umma yawe yanatoa gawio kuliko kwenda kuchukua raslimali hazina jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya taasisi na Taifa kiujumla,”alisema Kichere
Hata hivyo ,Kichere alisema kuwa ofisi ya Ukaguzi ipo wazi na itaendelea kushirikiana kikamilifu na ofisi ya msajili ili kuhakikisha makubaliano waliyofikia yanafanikiwa na hivyo kuyafanya mashirika ya Umma kusongambele.

More Stories
Tuzo za EAGMA zazinduliwa rasmi
Katibu Mkuu Nishati aipongeza Sweden kufadhili miradi ya umeme nchini
RAS Seneda akabidhi msaada wa Mablanketi kwa wazee na yatima