Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Tunduma.
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, amewataka wanafunzi kusoma kwa bidii ili kupata maarifa yatakayowasaidia katika maisha yao ya baadaye.
Kikwete alitoa rai hiyo, Februari 25, 2025, wakati akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Uwanjani iliyopo katika Halmashauri ya Mji Tunduma, mara baada kufanya ukaguzi na kuzindua jengo la ghorofa, wakati wa ziara yake katika Shule hapo.
Shule hiyo ya ghorofa iliyojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.6, ina vyumba vya madarasa 12 na jumla ya wanafunzi 1014 .
Kikwete alisema kuwa ni furaha ya kila mzazi kuona mwanae akisoma na kupata mafanikio.
Aliwataka wanafunzi kutumia fursa hiyo ya kusoma katika mazingira bora ya kujifunzia yanayoendelea kuimarishwa na serikali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Songwe, Radwell Mwampashi, alieleza kuwa serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa katika kuboresha miundombinu ya elimu.
Alisema kuwa ujenzi wa shule kama Uwanjani, yenye madarasa ya ghorofa, ni hatua kubwa kwani miundombinu ya majengo kama hayo ni yanayotumiwa na wanafunzi wa vyuo vikuu kwenye baadhi ya mataifa.
“Miundombinu kama hii hutumiwa na wanafunzi wa vyuo vikuu katika mataifa mengine, hivyo ni hatua kubwa kwa elimu ya Tanzania,” alisema Mwampashi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, alisema kuwa ujenzi wa shule hiyo kwa mtindo wa ghorofa umeongeza idadi ya madarasa, hivyo kusaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi.
Awali taarifa iliyotolewa na Halmashauri ya Mji Tunduma chini ya Kaimu Mkurugenzi Innocent Maduhu, ilieleza kuwa mbali na jengo hilo, miundombinu mingine iliyojengwa katika mradi huo ni Ofisi mbili za walimu, matundu 24 ya vyoo, Maabara tatu za Sayansi, Jengo la Utawala moja, Maktaba, chumba cha
Tehama, Kisima kirefu, pamoja na nyumba moja ya walimu inayotumiwa na familia mbili (Two in One).
Taarifa hiyo iliongeza kuwa, licha ya mafanikio haya, bado kuna changamoto ya upungufu wa walimu. Shule inahitaji walimu 442, lakini waliopo kwa sasa ni 315.



More Stories
Tanzania kuchimba visima vya utafutaji Mafuta Eyasi Wembere
Watafiti wa mimea vamizi watua Serengeti
Meya akabidhi Televisheni na king’amuzi Yanga