February 25, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwanza wahimizwa kutumia bidhaa zinazozalishwa na kampuni za kizawa

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Wananchi wa Mkoa wa Mwanza wamehimizwa kujenga na kukuza utamaduni wa kununua na kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini na kampuni za kizalendo(kizawa), ikiwemo za ALAF,ili kukuza uchumi wa taifa.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda, Februari 24,2025, wakati akizindua duka la maonesho ya mabati na vigae vya kuezekea nyumba(showroom) ya kampuni ya ALAF eneo la Buzuruga jijini Mwanza.

Ambapo amesema kampuni ya ALAF inaendeshwa kwa ubia kati ya kampuni mama ya SAFAL Group na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ina hisa asilimia 24,katika uwekezaji wa kampuni hiyo.

“Wananchi wa Mwanza na mikoa ya Kanda ya Ziwa niwasihi tumueni bidhaa zinazozalishwa na kampuni ya ALAF katika miradi ya Serikali na binafsi,na tutakuwa tunachangia mapato ya Serikali kwani kila faida itakayotengenezwa kila mwaka asilimia 24 ya faida hiyo itaingia kwenye mfuko wa Serikali yetu,” amesema Mtanda na kuongeza:

“Kwaio nyinyi mkinunua na mkaleta wateja wakanunua mabati,vigae na vitu vingine,maana yake umeiwezesha Serikali kupata fedha na kodi,hivyo kuchochea uchumi na maendeleo ya taifa pamoja na kusongeza huduma karibu kwa wananchi katika sekta ya ujenzi,”.

Amesema kampuni hiyo imejenga mtambo wa kuzalisha bati za rangi nchini mwishoni mwa mwaka 2024,pia imetoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 1500 hadi 2000 waliopata ajira za kudumu na wale wanafanya kazi kwa siku wapo wa kutosha,hivyo imesaidia Serikali kutatua tatizo la ajira nchini na wananchi.

Pia amesema,Serikali itaendelea kujenga Tanzania ya viwanda kwa kuweka mazingira rafiki katika sekta ya viwanda na kukuza ushirikiano na kila mmoja ambaye atawekeza juhudi zake taifa itapiga hatua moja mbele.

Sanjari na hayo Mtandao,amesema Mkoa wa Mwanza unauwekezaji wa miradi yenye thamani ya zaidi ya tirioni 5.6,ambazo zimeletwa na Serikali Kuu ikiwemo ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi(J.P.Magufuli) lenye thamani ya bilioni 600, upanuzi wa uwanja wa ndege bilioni 13 utakuwa uwanja wa kimataifa.

Hivyo miradi hiyo yote ikikamilika itakuwa na uwezo wa kuimarisha uchumi wa Mkoa wa Mwanza na kuongeza uchangiaji wa pati la Taifa kutoka asilimia 7.2 hadi kufikia asilimia 10 kwa mwaka ujao.

Kwa upande wake Meneja Masoko wa kampuni ya ALAF Isamba Kasaka,amesema kampuni hiyo ni ya kizawa ambayo imekuwa ikitoa huduma katika sekta ya ujenzi takribani miaka 60.

“Mkoa wa Mwanza unakua,hivyo tukaona vyema kuunga mkono juhudi za Serikali katika kusogeza huduma kwa wananchi ili waweze kupata huduma bora na kwa wakati,”amesema Isamba.

Naye Mkuu wa kitengo cha Biashara wa kampuni ya ALAF,Sateesh Yamsani,amesema wameona uwezo wa kuunga mkono ajenda ya Serikali katika uchumi hivyo wakaamua kupanua wigo wa usambazaji wa bidhaa za ujenzi kwa kuanzisha duka hilo ‘showroom’,eneo hilo la Buzuruga mkoani Mwanza kwa ajili ya utoaji huduma kwa haraka.

Pia kuonesha fursa za kiuchumi za Mkoa wa Mwanza ili kuunga mkono maendeleo ya kiuchumi.