Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
MKURUGENZI wa shirika la Kivulini,Yasin Ally, amesema ili vijana wa Kiislamu wapate maendeleo na kushindana kimataifa,ni muhimu BAKWATA na Jumuiya ya Kuendeleza Qu’ran na Sunna Tanzania (JUQUSUTA), kubadili mifumo ya elimu ya madrasa, ikiwemo kuingiza lugha ya Kiingereza katika ufundishaji wa Qur’an.
Yasin amebainisha hayo katika kongamano la vijana wa Kiislamu mkoani Mwanza,lililoandaliwa na JUQUSUTA kwa ajili ya kupokea mwezi Mtukufu wa Ramadhani,ambapo amesema viongozi wa BAKWATA na jumuiya za Kiislamu wanatakiwa kuongeza juhudi za kiuchumi na kiufundi kwa walimu wa madrasa.

Amesema JUQUSUTA itoke katika sifa na vigezo vya sasa vya kuwapata walimu wa madrasa ili kuwasaidia watoto wa Kiislamu,badala ya kuwakaririsha Qu’ran kwa Kiarabu,itumike lugha ya Kiingereza kuwawezesha kushindana kimataifa.
“Uendelezaji wa Qu’ran kwa Kiarabu hautakuwa na tija,tengenezeni mifumo mipya ya ujenzi wa walimu wa madrasa waendane na hali ya sasa, tuwafundishe Kiingereza watoto wa Kiislamu hapo tutakuwa tumewasaidia,”amesema Yasin na kuongeza;
Pia, amesisitiza kuimarisha stadi za kiuchumi kwa walimu wa madrasa ili kuweza kufikia malengo ya kimaendeleo ya BAKWATA na uislamu, huku akitahadharisha endapo wataendelea kutegemea mfumo wa sasa, walimu wa madrasa watakuwa tegemezi na hawatakuwa na uwezo wa kujikimu kiuchumi.
Akizungumzia umuhimu wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) amesema ni fursa kwa maendeleo ya Uislamu, na akazitaka taasisi hizo kuandaa mikakati ya kuwawezesha vijana na walimu katika nyanja hizo.

Kwa upande wake, Mlezi wa JUQUSUTA Sheikh Hasani Kabeke, amesema kongamano hilo linawalenga vijana wa Kiislamu,ambao wengi wao wapo mitaani na wanakosa ajira au nafasi ya kushiriki kwenye maendeleo ya jamii.
Ameonya kuhusu hatari ya vijana kushawishika kufanya fujo au kuhusika na maandamano ya kisiasa,huku akisisitiza kuwa lengo la kongamano hilo ni kulinda amani na utulivu wakati wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Sheikh huyo wa Mkoa wa Mwanza,ameonya kuelekea uchaguzi mkuu asitokee mtu wa kuwahamasisha vijana kuandamana,kufanya fujo na kugomea uchaguzi, wakatae kwani watakaodhurika ni vijana walio mitaani wakiwemo waislamu.
“Tunaowajibu wa kuwalinda na kukemea vijana,kwa sababu lengo letu ni kulinda amani na utulivu na kuiombea nchi kama ilivyo kauli mbiu ya kongamano hili ‘Kuna Maisha baada ya Uchaguzi;Linda Amani,Chagua kwa Hekima,”amesema Sheikh Kabeke na kuongeza:
“Ninatoa wito kwa jamii ya Kiislamu kuungana ili kuhakikisha vijana wanapata elimu bora, ujuzi na fursa za kiuchumi waweze kujitegemea na kuwa na mchango katika maendeleo ya taifa,”amesema Sheikh Kabeke.

More Stories
Mwanza wahimizwa kutumia bidhaa zinazozalishwa na kampuni za kizawa
TEA yatenga bil.3 kufanikisha utekelezaji mtaala mpya wa elimu
Mama Samia Legal Aid Campaign yawa mkombozi kwa wananchi Mbeya