Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online,Songwe
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwan Kikwete, ameahidi kufuatilia mchakato wa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mbalizi – Mkwajuni hadi Makongolosi,yenye urefu wa kilometa 128.
Ambapo amesema anatambua umuhimu wa barabara hiyo kwa uchumi na maisha ya wakazi wa Songwe na mikoa jirani.

Kikwete amezungumza hayo Februari 24, 2025, mara baada ya kukagua ujenzi wa madarasa sita katika shule ya sekondari Kanga, akiwa katika ziara wilayani Songwe, amesema barabara hiyo ni kiunganishi muhimu cha Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na mikoa ya Kati na ya Kanda ya Ziwa, hivyo ni lazima iharakishwe ili kurahisisha usafiri na kuchochea biashara.
“Badala watu wanaotoka Mbeya au Songwe kulazimika kuzunguka hadi Iringa kwenda Singida, barabara hii ikikamilika itarahisisha safari,kwani watakatiza hapa hadi Makongolosi na kuelekea mikoa mingine ya Kati na Kanda ya Ziwa,”amesema Kikwete.
Amesema mkandarasi ameshapatikana na mazungumzo yamefanyika,hivyo ndani ya mwezi mmoja ataanza kuleta vifaa na kazi itaanza rasmi ifikapo Juni mwaka huu.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Songwe, Mhandisi Joseph Mayaya, ameeleza kuwa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 128 itaanza kwa awamu ya kwanza kwa kujengwa kilometa 10 kwa kila Mkoa ambapo barabara hiyo ya Songwe na Mbeya.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Solomon Itunda,amesema Wilaya hiyo imeendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato, ambapo matarajio ni kukusanya bilioni 4.6 katika mwaka huu wa fedha.
Amesema kwa upande wa TARURA Wilaya hiyo imepokea shilingi bilioni 8 kwa ajili ya ujenzi wa mtandao wa barabara za lami katika mji wa Mkwajuni, makao makuu ya wilaya hiyo.
Huku sekta ya afya imenufaika kwa kupokea shilingi bilioni 12, huku sekta ya barabara ikipatiwa shilingi bilioni 9 ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia.

Kwa upande wake , Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Cecilia Kavishe,amesema Halmashauri ilipokea kiasi cha shilingi milioni 150 kwa ajili ujenzi wa madarasa,lengo likiwa ni kupunguza msongamano wa wanafunzi shule ya sekondari Kanga yenye jumla ya wanafunzi 1200 wa kidato cha kwanza hadi sita.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Songwe, Radwell Mwampashi, amesema hali ya kisiasa mkoani humo iko shwari, huku viongozi wa Serikali na chama wakishirikiana kuhakikisha wanaleta maendeleo kwa wananchi.
Katika ziara yake ya siku tatu mkoani Songwe, Kikwete anatarajiwa kukagua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 700, ikihusisha sekta za elimu, afya, na miundombinu.

More Stories
Rais Samia aridhishwa na utekelezaji miradi Tanga
Ziara ya Rais Samia yaanza kwa kishindo mkoani Tanga
Gambo: Rais Samia amefanya makubwa Jimbo Arusha Mjini