Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
WAKALA ya Barabara Tanzania(TANROADS)imesema katika kipindi cha miaka minne, hali ya barabara kuu na za mikoa imeendelea kuimarika ambapo barabara zilizo katika hali nzuri na wastani zimekuwa karibu asilimia 90 ya jumla ya mtandao wote wa barabara wenye Kilometa 37,225.72.Â
Imesema katika kipindi cha miaka minne(2021-Februari 2025) ya Serikali ya Awamu ya Sita barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 1,365.87 zimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami na barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 2,031.11 zimeendelea kujengwa kwa kiwango cha lami.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Februari 17,2025 na Mkurugenzi wa Mipango ya Miundombinu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS),Mhandisi Ephatar Mlavi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya serikali ya awamu ya sita katika sekta ya ujenzi.
Amesema kuwa katika kipindi hicho barabara zingine zenye urefu wa jumla ya kilometa 15,625.55 zipo katika hatua mabalimbali za utekelezaji.Huku barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 2,052.94 na madaraja mawili (2) zimefanyiwa Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina na Serikali inatafuta fedha za kuzijenga kwa kiwango cha lami na upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara zenye jumla ya kilometa 4,734.43 na madaraja kumi unaendelea.
Aidha amesema kuwa Miradi ya barabara yenye urefu wa takriban kilometa 5,326.90 na miradi saba ya madaraja ipo katika hatua ya manunuzi kwa ajili ya kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ikiwa ni maandalizi kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara hizo kwa kiwango cha lami.

“Jumla ya madaraja makubwa 9 yamekamilika kujengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 381.301 na madaraja mengine kumi ujenzi wake unaendelea kwa gharama ya shilingi Bilioni 985.802. Jumla ya madaraja makubwa 19 yapo kwenye maandalizi ya kujengwa.
Akizungumzia Mafanikio mengine yaliyopatikana katika sekta ya barabara Mhandisi Mlavi amesema ni kumalizika kutekelezwa kwa miradi ya miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), Awamu ya Pili KM 20.3 (Mbagala – Mzunguko wa Bandari (Bendera Tatu), Bendera Tatu – Kariakoo, Sokoine – Zanaki, Barabara ya Kawawa – Barabara ya Morogoro (Magomeni).
“Kuendelea kutekelezwa kwa miradi ya miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), Awamu ya Tatu (3) KM 23.3 katikati ya jiji hadi Gongo la Mboto ambao umefikia asilimia 74, Awamu ya Nne ya mradi huo KM 30.1 kutoka katikati ya jiji hadi Tegeta ambao umefikia asilimia 22.
“Ujenzi wa awamu ya tano kutoka Ubungo – Bandarini na Segerea – Tabata – Kigogo, km 25.4 upo katika hatua za mwisho za manunuzi,”amesema.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali,Gerson Msigwa amesema kuwa Taasisi za Serikali zimeanza kuzungumza na vyombo vya habari kuanzia leo Februari 17, 2025 hadi Februari 27, 2025 na baada ya hapo, Machi 14, 2025,Mawaziri wataanza kuzungumza na vyombo vya habari.
“Ifikapo tarehe 19/03/2025, Serikali ya Awamu ya Sita itakuwa inatimiza miaka minne tangu ilipoingia madarakani, Idara ya Habari hivyo Nawasisitiza viongozi wa Taasisi za Umma kuja kutoa taarifa za utendaji wa taasisi zao ndani ya miaka minne, wasiotekeleza hilo watatakiwa kueleza sababu za kutofanya hivyo,”amesema Msigwa.

More Stories
Kamati ya kudumu ya Bunge ya utawala,katiba na sheria yaridhishwa ujenzi soko Kariakoo
TRA Tanga yakusanya bil.178.3 kwa miezi sita
Wataalam Sekta ya utalii watakiwa kufanya kazi kwa uadilifu,kujituma na kuwa wabunifu