Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Mwanza
Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limetakiwa kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao ikiwemo kudhibiti uhalifu katika miradi ya kimkakati inayotekelezwa.
Huku Maofisa Wakaguzi na Askari waliofanya kazi nzuri na kunutunukiwa vyeti vya sifa na zawadi,wametakiwa kutobweteka na badala yake waendelee kufanya kazi kwa bidii, nidhamu,weledi,kujituma na kutoa huduma inayozingatia haki kwa wananchi.
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/Screenshot_20250209-131245.png)
Hayo yameelezwa Februari 8,2025 na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Said Mtanda,katika siku ya Familia ya Polisi (Polisi Family Day),ambapo aliwatunukua vyeti na zawadi, Maofisa Wakaguzi na Askari waliofanya kazi nzuri zaidi mwaka 2024,iliofanyika uwanja wa Mabatini Polisi, wilayani Nyamagana mkoani Mwanza.
“Endeleeni kulinda miradi ya kimkakati inayotekelezwa mkoani Mwanza,likiwemo daraja la Kigongo-Busisi,linalogharimu zaidi ya bilioni 700,wapo wajinga wachache wanakwenda kuiba vyuma na kuviuza, SGR napo wahalifu wengi wanajipanga kuhujumu reli,mjipange kuwadhibiti wasihujumu uchumi wetu,”amesema Mtanda.
Amesema wakaguzi ni uti wa mgongo wa Jeshi la Polisi,hivyo amewataka kuendelea kufanya kazi ya kukomesha mauaji ya watu wenye ualbino,biashara na matumizi ya dawa za kulevya,mauaji ya kujichukulia sheria mkononi,makosa ya mtandaoni na usalama barabarani.
Pia amesema Serikali imefanya uboreshaji wa Jeshi la Polisi,kuwapandisha vyeo Askari,kukarabati vituo vya polisi na kuongeza vitendea kazi (magari),hivyo kuimarisha Kamisheni ya Polisi Jamii na kupeleka wakaguzi kuhudumia wananchi katika Kata zote ni mafanikio kwa jeshi hilo.
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/Screenshot_20250209-131320.png)
Awali Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,Naibu Kamishna wa Polisi (DCP),Willbrod Mutafungwa, amesema Askari 18 na Wakaguzi 4,wametambuliwa kwa juhudi na utendaji kazi wao kwa mwaka 2024,hivyo wamewatunukia vyeti na zawadi ili kuwapa motisha na kuongeza chachu.
Mutafungwa amesema,siku hiyo ni adhimu ambapo hupata fursa ya kukaa na familia zao na kufurahi pamoja,mwaka jana walisitisha likizo na shughuli zingine ili kuhakikisha wananchi wanakaa kwa amani na walimaliza vyema mwaka mpya.
“Katika siku hii,tunapata nafasi ya kutafakari tuliyofanya na tunakokenda,mwaka huu tunakwenda kwenye uchaguzi mkuu, tunaendelea na maandalizi ya kujipanga na uchaguzi ufanyike kwa amani na usalama kama ilivyokuwa uchaguzi wa serikali za mitaa 2024,”.
Pamoja na hayo amesema,kwa sababu askari ni washiriki wa uchaguzi,wameanza kupata mafunzo ya utayari na usimamizi wa uchaguzi,ambapo Maofisa 19 wakiwemo Wakuu wa Polisi wa Wilaya, Wakaguzi 110 na Askari 185 kutoka Wilaya mbalimbali mkoani hapa wanaendelea na mafunzo hayo.
Amesema mafunzo hayo yatakayofanyika kwa awamu mbili,ni maelekezo ya IGP ya kuwataka kufanya maandalizi mapema kabla na wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2025.
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/Screenshot_20250209-131302.png)
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/Screenshot_20250209-131129.png)
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/Screenshot_20250209-131331.png)
More Stories
Shule ya Hollyland yafagiliwa ubora wa taaluma
Dkt.Kiruswa: Tanzanite kuuzwa ndani, nje ya Mirerani
Jamii yatakiwa kutafsiri maendeleo yanayofanywa na Rais