February 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waumini K.K.A.M watoa kilio chao kwa Rais Samia

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

WAUMINI wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (K.K.A.M) Kata ya Makwale wilayani Kyela mkoani Mbeya, wamemuomba
Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuwasaidia wasizuiliwe kuabudu kwenye makanisa waliyojenga kwenye kaya zao.

Akizungumza na TimesMajira Online mmoja wa waumini wa kanisa hilo Kata ya Makwale, Elen Msopa, amesema watu ambao wanawazuia kuabudu kwenye makanisa yao hawajulikani kama wapo kwenye kaya zao na kama wapo basi waonekane wafahamike.

Inadaiwa kuwa Bodi ya wadhamini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT Dayosisi ya Konde ndio wanawazuia waumini wa kanisa la K .K.A.M kuabudu kwenye maeneo yao bila kuainisha sababu za msingi juu ya haki hiyo ya uhuru wa kuabudu.

Msopa amesema kuwa shauri la ardhi namba 24 la mwaka 2023,katika Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Kyela,lilitupiliwa mbali shauri hilo na Mwenyekiti wa Baraza,na kuelekeza upande usioridhika na uamuzi wa baraza ukate rufaa ndani ya siku 30,lakini badala ya kukata rufaa waliambiwa wasimame kuendelea na ibada katika makanisa hayo.

“Tunashangaa kimetokea nini cha kutaka tuondolewe kwenye makanisa yetu,wakati shauri namba 24 la ardhi la mwaka 2023 ile hukumu ilitupa ushindi sisi (K.K.A.M). Tunamuomba Rais Dkt.Samia atusaidie, maeneo haya ni asili yetu twende wapi sasa,” amesema Msopa.

Muumini mwingine wa usharika wa Isimba Kata ya Makwale, Tupokigwa Kisisiri, amesema alizaliwa mwaka 1969 na kukuta kanisa lipo na kuonesha kushangazwa na watu wanaojitokeza kusema makanisa hayo ni yao.

“Tunaomba Rais Dkt.Samia utusaidie maana kanisa hili ni mji wetu,hatukuchanga fedha na sio kwamba Dayosisi ilitusaidia kuchanga fedha, huu ni Mji wa mzee wetu Andamwile na kujenga amejenga mtoto wetu wala hatukuona mchango wowote,”amesema Kisisiri.

Eliezery Ngailo kutoka usharika wa Ngeleka, amesema kuwa maeneo yote yaliyojengwa makanisa walipewa na mababu zao, lakini cha ajabu suala limegeuka kuwa shida na kufanya sehemu ya kuabudia kwao kuwa changamoto na kuishi kama wakimbizi licha ya kuwa maeneo yao.

Aston Mwalundilin kutoka usharika wa Eden, amesema kwamba eneo hilo lilipatikana mwaka 1968 wakati walifikiri wapi wajenge eneo la kanisa,hivyo waliwafikia wazee wawili ambao walikubaliana kuwapatia eneo kwa ajili ya kuabudu na kugawa eneo lenye ukubwa wa hekali robo tatu.

Akizungumzia sakata hilo Katibu Mkuu wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Konde, Benjamin Mbembela amesema kuwa amri ilitolewa waumini wa K.K.A.M na KKKT wasitumie makanisa hayo lakini cha ajabu wenzao bado wanayatumia .

“Kesi hii iliondolewa kwa mapungufu ya kisheria mahakamani,na madai ya kusema sisi tumewazuia sio kweli,lakini kitu kingine wao walipoitwa walidai wanaohusika si wao hivyo ikabidi wakili wa K .K.A.M apeleke shtaka lingine,”amesema.