Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
KATIKA kuadhimisha miaka 48 ya Chama Cha Mapinduzi(CCM),Chama hicho kinatarajia kuwatambulisha Rasmi wagombea wake katika nafasi ya ngazi ya Urais na Makamo kwa wanachama wake Januari 5,2025 jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo,Januari 3,2025 Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa CPA.Amos Makalla amesema kuwa jambo kubwa katika sherehe hizo ambapo Mweyekiti wa Chama hicho ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi litakuwa ni kuwatambulisha wagombea wa Urais na Makamu wa Rais Tanzania bara na Tanzania Visiwani.
“CCM inafanya sherehe yake ya kutimiza miaka 48 tangu kuzaliwa kwake na katika tukio hilo jambo kubwa ni kuwatangaza wagombea ambao walipitishwa na mkutano mkuu kugombea nafasi ya Urais na makamu ya Rais kwa Tanzania bara pamoja na mgombea Urais kwa Tanzania visiwani.
“Ijulikane kuwa kwa sasa CCM inawatangaza wagombea wao kwa wana CCM na muda ukifika watambulishwa kwa wananchi ili kufanikisha suala la kutimiza masuala ya uchaguzi kikatiba lakini sasa hivi ni muda wa wanachama wa CCM kutambilishwa wagombea wao,”amesema Makalla.
Aidha CPA Makalla amewataka wana CCM wote kutoka mikoa ya jirani na walioko katika Dodoma kuhakikisha wanafika katika uwanja wa Jamhuri kwa ajili ya kushuhudia sherehe hizo .
“Niwakaribishe watanzania wote walioko Dodoma na nje ya Dodoma wana CCM na wasiokuwa wana CCM kufika katika uwanja wa Jamhuri kwa kuwa milango itakuwa wazi kuanzia saa 12 alfajiri hii siyo ya kupewa kadi kila mtu anakuja,”amesema.
Chama hicho ambacho kinatimiza miaka 48 tangu kianzishwa kinatarajiwa kufanya sherehe zake katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma,sherehe hizo zitakuwa na viongozi mbalimbali ndani ya CCM na nje ya CCM.
More Stories
Mwabukusi:Kufanyakazi kwa kushirikiana na serikali siyo kulamba asali
Waislamu wamuombea dua Rais Samia,wasisitiza umoja
Samia: Serikali imejifunza somo kuporomoka ghorofa