February 2, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU yadhibiti zaidi ya milioni 360

Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

TAASISI ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU),Mkoa wa Mwanza imefanikiwa kudhibiti na kuokoa kiasi cha milioni 366.9 za ukusanyaji wa kodi ya zuio zisichepushwe.

Pia,imefuatilia miradi 13 ya maendeleo inayogharimu kiasi cha bilioni 4.4 katika sekta za elimu,barabara na biashara ambapo kati ya hiyo,miradi 12 yenye thamani ya bilioni 3.9 ilikutwa na dosari mbalimbali.

Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza,Idrisa Kisaka, ameeleza Februari Mosi,2025,wakati akitoa kwa waandishi wa habari taarifa ya robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/25.

Amesema katika kipidi cha Januari hadi Desemba 2024,TAKUKURU ilifanikiwa kudhibiti kiasi cha milioni 366.9 za kodi ya zuio katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mnada wa Mifugo,wilayani Misungwi,zisiingie mifukoni mwa watu.

Kisaka amesema ilifuatilia miradi 13 ya maendeleo,kati ya hiyo miradi 12 yenye thamani ya sh.bilioni 3.9 ilikuwa na dosari,hivyo yalitolewa mapendekezo 46 ya kuiboresha ambapo 30 yametekelezwa.

“Ufuatiliaji huo wa TAKUKURU umesaidia utekelezaji wa mapendekezo kwa asilimia 65.2 na kuwezesha miradi hiyo kutekelezwa kwa ubora wa kiwango kilichokusudiwa,”amesema.

Pia,ilichambua mfumo ili kubaini mianya ya rushwa katika usimamizi wa Jumuiya za Maji ngazi ya Jamii,makusanyo ya ushuru wa mazao ya uvuvi,mianya ya rushwa katika utoaji wa leseni za biashara na mfumo wa ukusanyaji mapato kwa mashine POS.

“Chambuzi hizo zilisababisha warsha kufanyika na kutolewa mapendekezo 16 ambayo yametekelezwa kwa asilimia 87.5.Elimu kwa umma makundi mbalimbali yamefikiwa ikilenga ushirikishwaji wa wadau katika mapambano dhidi ya rushwa,”amesema Kisaka.

Kwa mujibu wa Kisaka,makundi hayo ni ya waandishi wa habari,viongozi wa dini,taasisi za umma na zinazosimamia utawala bora,Asasi za kiraia,Sekta Binafsi,wavuvi,wajasiriamali,wafanyabiashara,wakulima,wafugaji,bodaboda,wazee maarufu na wananchi.

Amesema Oktoba-Desemba 2024,TAKUKURU mkoani Mwanza,ikishirikiana na wadau ilifanikiwa katika mapambano dhidi ya rushwa kupitia uchambuzi wa mfumo,ufuatiliaji miradi ya maendeleo,elimu kwa umma,utekeleza wa programu ya TAKUKURU Rafiki,uchunguzi na mashitaka.

Kisaka ameeleza kuwa katika kipindi hicho cha Oktoba-Desemba, malalamiko 60 yalipokelewa,34 hayakuhusiana na rushwa,26 yalihusu vitendo vya rushwa ambapo majalada manne yamekamilika.

Ambapo majalada hayo manne yamepata kibali cha Ofisi ya Mashitaka,kesi sita zimefunguliwa mahakamani, huku Jamhuri ikishinda kesi 10 katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2024.

Aidha,wananchi katika Kata 19 wamenufaika kupitia Programu ya TAKUKURU Rafiki baada ya watoa huduma kutatua kero 46 kati ya 154 zilizoibuliwa,ili kuboresho huduma katika sekta za elimu,afya,maji,nishati na barabara.