January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANAPA yatoa mafunzo usimamizi wa moto kwa JWTZ Mikumi

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), limeendesha mafunzo maalum ya usimamizi wa moto kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi mkoani Morogoro.

Mafunzo hayo yaliwalenga wanajeshi wa Kikosi cha Usafiri wa Anga 603 kutoka Dar es Salaam, chini ya uongozi wa Meja Samson Ngowe, kwa lengo la kuwapa ujuzi wa kukabiliana na changamoto za majanga ya kitaifa, hususani moto pori.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa Uhifadhi Daraja la Kwanza Samwel Mgohach amebainisha kuwa moto pori ni moja ya changamoto kubwa zinazoathiri hifadhi za taifa. Moto huo mara nyingi husababishwa na radi, ujangili, na matumizi yasiyo makini ya moto karibu na Hifadhi.

Mafunzo hayo yaliangazia aina kuu tatu za moto ukiwemo, moto wa uso (surface fires), moto wa taji (crown fires), na moto wa ardhini (ground fires).
Jeshi hilo lilipatiwa mbinu za kuzima moto pamoja na njia za kuzuia majanga ya moto kwa kutumia teknolojia na mbinu za kisasa.

Aidha, Mgohach ameelezea umuhimu wa kutumia moto uliodhibitiwa (prescribed fires) kama njia ya kudhibiti mimea vamizi kama Lantana camara, kuboresha rutuba ya udongo na kuhakikisha bayoanuwai inabaki salama.

Pia, amesisitiza kuwa moto uliodhibitiwa husaidia kupunguza hatari ya moto usiodhibitiwa, ambao ni tishio kwa mifumo ya ikolojia na wanyamapori.

Akiizungumza katika mafunzo hayo Meja Samson Ngowe, ameishukuru TANAPA kwa kuwapa uzoefu kupitia mafunzo hayo na kuahidi ushirikiano wa karibu kati ya JWTZ na TANAPA katika kulinda Hifadhi za Taifa.

“Tunawashukuru kwa jitihada zenu za kuimarisha uhifadhi na kuhakikisha mazingira yetu yanabaki salama kwa vizazi vijavyo,” amesema Meja Samson.

Pamoja na mafunzo hayo Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) limepata fursa ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, ambapo walijionea uzuri wa mandhari yake na aina mbalimbali za wanyamapori.

Mafunzo hayo yanaonesha dhamira ya TANAPA ya kushirikiana na wadau mbalimbali katika kulinda rasilimali za Taifa.