Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Dar
Mwanasiasa mkongwe na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja, amewatakia heri wana-CCM katika mkutano mkuu wa kushika mikoba ya aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, Abdulahman Kinana.
Akizungumza Januari 16, 2025 jijini Dar es Salaam, amesema kuwa shauku kubwa ya wana-CCM ni kumpata Makamu Mwenyekiti atakayemsaidia Mwenyekiti wa chama hicho ambaye ni Rais Samia Suluhu Hassan.
“Nina imani kuwa atapatikana Makamu Mwenyekiti atakayemsaidia Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Samia, kwani CCM ina hazina kubwa ya viongozi na wenye uwezo wa kuongoza katika nyanja mbalimbali,” amesema Mgeja na kuongeza:
“Tunaamini kuwa atakayepatikana atakuwa ni mwenye kumshauri Mwenyekiti wa CCM, katika kuleta mabadiliko ndani ya chama hivyo ni vyema sasa tukasubiri mkutano mkuu wa CCM unatarajiwa kufanyika Januari 18 hadi 19, 2025, jijini Dodoma.
Kabla ya Mkutano Mkuu, kikao cha Kamati Kuu kimefanyika Januari 16, 2025, ambacho kitatoa mapendekezo rasmi.
Awali Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla amesema mkutano huo wa CCM utaambatana na vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa, ambapo ajenda zitahusu kufanya uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, kupokea taarifa ya utekelezaji wa kazi za chama kwa kipindi cha mwaka 2022 hadi 2025, pamoja na taarifa ya utekelezaji wa Ilani kwa pande zote mbili, Bara na Zanzibar.
Kuhusu mchakato wa kumrithi Kinana, amesema mrithi wa nafasi hiyo anatarajiwa kupatikana baada ya Kamati Kuu kuwasilisha mapendekezo ya jina kwa Halmashauri Kuu kisha jina hilo kuwasilishwa kwa wajumbe wa mkutano mkuu kwa ajili ya kupigiwa kura
More Stories
Hatua za kisheria kuchukuliwa kwa wanaohatarisha usalama Mbeya
Maofisa ujenzi Manispaa Tabora kikaangoni
Mbeya yapokea bil.23.4 ujenzi sekta ya elimu