Fresha Kinasa,TimesMajiraOnline,Mara.
WAZAZI wa Wanafunzi wa Kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari Muhoji Kata ya Bugwema ambayo ni Sekondari Mpya ya Kata hiyo katika Jimbo la Musoma Vijijini Mkoani Mara, wamekubaliana kuhakikisha wanachangia upatikanaji wa chakula cha mchana kwa wanafunzi wote kuwawezesha Watoto wao wasome kwa ufanisi.
Sekondari hiyo ambayo ilianza kujengwa kwa kutumia nguvu za wanavijiji, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini,baadhi ya Wazawa wa Kijiji cha Muhoji pamoja na Serikali kuu ambayo imechangia ujenzi wa Sekondari hiyo Shilingi Mil.75 imetajwa kuwa, iko tayari kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Januari 15,2025 imebainisha hayo ambapo Wazazi hao wamekubaliana katika kikao kilichofanyika Kijijini hapo mambo manne.
Ambapo Jambo la kwanza ni Wazazi kuchangia chakula Cha mchana kwa wanafunzi wote. Huku Jambo la pili likiwa ni Wazazi hao kukubaliana kuwa watanunua madawati ya watoto wao ambayo yanatengenezwa Kijijini hapo.
Jambo la tatu “Wazazi watahakikisha kuna uhusiano mzuri kati yao na Walimu, na Kati ya Wanafunzi na Walimu. Na Jambo la nne Wazazi wataendelea kushirikiana vizuri na Serikali kuhakikisha Sekondari yao inatoa elimu kwenye mazingira mazuri yenye mafanikio mazuri.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, miundombinu ya awali tayari imekamilishwa, ambapo ukamilishaji umefanywa kwenye vyumba vya madarasa, Ofisi za Walimu, Vyoo, maktaba na chumba vya matibabu.
Nao Wananchi wa Muhoji akiwemo Yunis Bwire ameshukuru kwa hatua hiyo kubwa ambayo amesema imechangiwa na Mbunge Prof. Muhongo kutoa hamasa kwa Wananchi kuchangia maendeleo, kutoa fedha zake binafsi, Fedha za Mfuko wa Jimbo na kushirikiana vyema na Serikali kukamilisha shule hiyo.
“Tunafurahi kwa sababu tunatambua fika kuwa, ili Watoto wafanye vizuri katika masomo yao lazima wapate Chakula, kwanza itasaidia hata mahudhurio yao darasani na kuongeza umakini wanapofundishwa na Walimu.” amesema Yunis Bwire.
Yunis ameongeza kuwa, shule hiyo itatatua changamoto kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza kutembea umbali mrefu wa kilometa 10, kwenda Masomoni kwenye Sekondari ya Kata iliyoko Kijijini Masinono.
Jimbo la Musoma Vijijini lenye Kata 21, lina Sekondari za Kata 26, na 2, za Binafsi. Sekondari mpya 6 zimepagwa kufunguliwa mwaka huu. Matayarisho ya kuanza ujenzi wa sekondari nyingine sita (6) Jimboni humo yamekamilika.
More Stories
Wasanii wa ‘Comedy’ kuwania tuzo
Jokate achangia milioni 3 mfuko wa bodaboda
Wizara ya Nishati yawasilisha utekelezaji wa bajeti 2024/2025 kwa Kamati ya kudumu ya bunge Nishati na Madini