January 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mhandisi Kundo agoma kuweka jiwe la msingi mradi wa maji

Na Mwandishi Wetu

NAIBU Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, amegoma kuweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa Vwawa-Mlowo uliopo Mkoani Songwe, unaotekelezwa na Mkandarasi Mzawa wa kampuni ya Current Construction Ltd ya Jijini Dar es salaam mpaka changamoto zilizopo zitakapo tatuliwa.

Mhandisi Kundo amesema kuwa, changamoto hizo ni pamoja na kazii kufanyika chini ya kiwango kilichokubaliwa.

Kufuatia hali hiyo, Mhandisi Kundo ameiagiza bodi ya Vwmwassa na RUWASA kuhakikisha kwamba wanamsimamia mkandarasi huyo, ili aweze kufanya marekebisho kwa kasoro zote zilizobainika.

Mhandisi Kundo amechukua uamuzi huo leo Januari 14, 2025 katika siku ya pili ya ziara yake ya siku mbili Mkoani Songwe, baada ya kusomewa taarifa ya maendeleo ya utekeleza kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vwawa-Mlowo (Vwamwassa), Mhandisi Clavery Casmir.

“Niko tayari kupewa majina mabaya, lakini kwa mradi huu siwezi kuweka jiwe la msingi mameneja wa Wilaya, hata mngekuwa mnatekeleza wenyewe, msingefanya kazi chafu kama hii,

“Hatuwezi kuona Rais analeta fedha zaidi ya shilingi bilioni 2 ili kutatua changamoto za wananchi, halafu mradi unakosa ubora na kuwa changamoto,hizo ni lazima ziondolewe kwanza, ndipo nitakuja kuuzindua rasmi,” ameongeza Mhandisi Kundo.

Mradi huo unahusisha kazi mbalimbali kama uchimbaji wa kisima cha maji eneo la Hasanga, ujenzi wa matenki mawili ya maji yenye ujazo wa lita 250,000 na 75,000, ulazaji wa mabomba yenye urefu wa mita 51,600, na ununuzi wa vifaa mbalimbali kama transifoma, jenereta, na pikipiki tano kwa ajili ya usimamizi.

“Serikali inaamua kuwapa wakandarasi wa ndani fursa ya kujenga uchumi wao, lakini wanapaswa kuhakikisha kazi zao zinakidhi viwango vilivyowekwa” amesema Mhandisi Kundo

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Vwamwassa, Simon Mboya, alikubaliana na hatua iliyochukuliwa na Naibu Waziri huyo na kuahidi kuwa suala hilo litawasilishwa kwenye vikao vya bodi kwa. maamuzi zaidi.

Mradi huo, ulianza Machi 2023, ulikuwa ukamilike Februari 2025, lakini changamoto hizo zimeweka shaka juu ya kukamilika kwa wakati Mradi huo, ambapo kukamilika kwa mradi huo kunatarajia kunufaisha zaidi ya wananchi 23,000 wa kata sita katika Wilaya ya Mbozi.