*Akunwa jinsi malengo ya Mapinduzi Matukufu yanavyosimamia, ajivunia mafanikio sekta ya elimu, akoshwa ujenzi Sekondari Bumbwini
Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline, Zanzibar
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemshukuru Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa uongozi safi na maono ya maendeleo anayofanya ndani ya nchi.
Rais Samia alitoa kauli hiyo jana visiwani Zanzibar wakati wa hafla ya uzinduzi wa Shule ya Sekondari Bumbwini Misufini ikiwa ni mwendelezo wa Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Aidha, Rais Samia aliwapongeza wananchi kwa kuwa tayari kuunga mkono juhudi za Serikali kuwaletea maenedeleo. Pia, Rais Samia alipongeza hatua ambayo wamefikia, akisema hayo ndiyo yalikuwa malengo ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Alisema walikuwa wanaenda hatua baada ya hatua na mwaka jana, wamefika hapo, lakini nako si padogo.
“Wazee wetu waliweka misingi mizuri sana. Waliona jambo la kwanza ni kusoma. Na wazee walivyoleta mapinduzi wakasema ni elimu bure kwa watoto wetu.
Mimi wakati Mapinduzi yanakuja nina miaka minne, bado sijaenda shule,” alisema Rais Samia na kuongeza;
“Mwaka 1965 ndipo nilipoanza kukanyaga banda la Skuli (shule) na nilikuwa sitatimiza umri, Baba yangu alikuwa mwalimu pale Kidoti, akitoka asubuhi natoka naye naingia darasa la kwanza, kwa hiyo mwaka 1965 nilikuwa nasoma darasa la kwanza, lakini mabanda yale ndiyo watoto wetu siku hizi wanaita mabanda ya mbunzi.”
Yalikuwa ya makuti, tulikuwa tunaingia tunasoma, darasa la pili nimesoma Chwaka, angalau yalikuwa na saruji (sakafu) tukaendelea hivyo, lakini baada ya sisi kupewa fursa na wazee tukasoma vizuri, tukajua maana ya elimu, awamu kwa awamu , tumekuwa tukiboresha elimu.”
Alisema waliokuja awamu ya pili wameboresha kwa kiasi chao, awamu ya pili, awamu ya tatu, hivyo hivyo kila awamu inaongeza mpaka wamefikia hatua hiyo.
Alisema ameweza kuingia kwenye madarasa ya shule ya Bumbweni, ndani ameona madarasa ya mtandao.
“Wakati naingia darasani nimekuta watoto wanasoma kwa njia ya mtandao, wameunganishwa na Taasisi ya Elimu Kibaha, darasa linafundishwa kule, wao wanafuatilia huku kila mtu kwa kompyuta yake.
Mapinduzi ni maendeleo hatua baada ya hatua, yale Mapinduzi ya kutafuta Uhuru tulimaliza sasa ni mapinduzi ya kuleta maendeleo na kulinda Uhuru wetu, ndiyo Mapinduzi yetu sasa hivi,” alisema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia alisema ndani ya shule hiyo ameona kuna maabara za kisasa sana. Alisema Fiziki ina maabara yake, Kemia ina maabara yake , vijana wanasoma.
“Huko nyuma tulikuwa tukifanya mitihani form four (kidato cha nne) Zanzibar usiitafute juu, uitafute chini utaiona iko wapi, utakuta ya pili kutoka chini, au imefanya vizuri zaidi ya nne kutoka chini, lakini sababu ilikuwa watoto hawakuwa wakifundishwa sawia, hatukuwa na maabara.
Sasa tumewajengea za kisasa , nilikuwa naongea na walimu mle ndani kwamba hatutaki kusikia ziro wala four (madaraja) .” Alisema
Aidha, alisema wameweka kompyuta darasani sio tu za wanafunzi, bali walimu wazitumie kuboresha ujuzi wao waingie kwenye kompyuta tafute ulimwenguni wanasomeshwaje.
Alisema kwa kufanya hivyo watakuwa walimu bora na maabara hizo zitatumika vizuri.
***Hali ya elimu kabla ya mapinduzi
Rais Samia alisema kabla ya Mapinduzi, Zanzibar na Pemba kulikuwa na shule 62 kati ya hizo za Sekondari zilikuwa tano na shule za awali ilikuwa moja.
“Lakini sasa hivi fikiriani kuna shule za awali ngapi , hiyo ni mwaka 1964. Kipindi hicho wanafunzi waliokuwa shule za awali, shule za msingi na sekondari walikuwa 25, 432, lakini sasa hivi tuna shule 1,308, lakini udahili wetu kwa wanafunzi waliokuwa shuleni mwaka jana (anataja takwimu zaidi 6.5) na kwa mwaka huu idadi utaongezeka,” alisema Rais Samia.
Pia alisema kuna vyuo ambavyo huko nyuma havikuwepo, ambapo anadhani vyuo vikuu Zanzibar wamevipata miaka ya 2000. Alisema sasa hivi wana vyuo vikuu na shule za michepuo na wana mfuko wa kusomesha watoto vyuo vikuu na kumuondea mzazi mzigo wa kusomesha mtoto katika mgazi hiyo.
“Hayo ndiyo matokeo ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, kwani lengo la Mapinduzi ilikuwa ni kustawisha hali za wananchi kielimu, kiafya, wapate maji safi na salama, wapate umeme ili wawe salama waweze kufanya mambo yao kwa salama na kwa amani,” alisema.
***Maono ya mbele
Rais Samia alisema hapo walipofikia wana maono ya mbele, ambayo ni kusomesha watoto wawe wataalam na sio tu wasomi. Aliongeza kusema kwamba unaweza ukawa msomi, ulichokisoma hakikusaidii wewe wala Taifa.
Lakini ukiwa mtaalam, huo utaalam utakusaidia wewe na Taifa lako. Alisema kama wasomi watatokea ni vizuri, lakini lengo letu ni kutayarisha wataalam watakaohimiri soko la ajira.
Alisema kwa sasa uwekezaji unaongezeka nchini na jana (juzi) alikuwa Bawe kuna hoteli ya kimataifa imetoa ajira 400, katika ajira zile alikuwa anaangalia watoto wanaofanana na Kipwapwani, kama wapo wachache sana.
“Hiyo inatuambia hatujafanya kazi nzuri sana kuzalisha wataalam katika sekta ya utalii na pengine kulikuwa na changamoto huko nyume, pengine mila zetu,” alisema.
Alisema kuna ajira za kitaalam, ajira za kawaida, lakini badala yake hawakupata wao, wamepata vijana wa Kitanzania.
Alisema kila uwekezaji unaokuja sasa unakuja kwa mitindo ya kutumia mitandao, mawasiliano ni mtandao, oda mtandao, sijui kitanda kimesafishwa ni mtandao, hivyo lengo lao ni kuzalisha vijana watakaoweza kuajirika.
More Stories
Kilo 673.2,dawa za kulevya zakamatwa Bahari ya Hindi
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali