January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watolewa hofu uvumi juu ya uwepo wa Teleza

Judith Ferdinand,Timesmajira Online, Mwanza 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewatoa hofu wananchi wa Mkoa huo,hususani wakazi wa  Kata ya Mkolani na Buhongwa,juu ya  uvumi ulioenezwa kwenye maeneo hayo zikieleza  uwepo wa mtu aitwaye Teleza, anayedaiwa kubaka, kuwalawiti wanawake na kuwajeruhi.

Huku Jeshi hilo likilaani kitendo cha baadhi ya wananchi waliojichukulia sheria mkononi, na kutaka kumshambulia mwananchi eneo la mtaa wa Ibanda, katika nyumba ya kulala wageni, Kata ya Mkolani, Wilaya ya Nyamagana.

Akizungumza Januari 8,2025 na wananchi wa maeneo hayo ,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa, amesema tukio hilo la wananchi kumshambulia mtu huyo,likitokea Januari 8,2025 majira ya saa nne asubuhi (10:00hrs),ambaye walifanikiwa kuokoa maisha yake.

Ambapo  chanzo cha kumshambulia mtu huyo,ni wananchi hao walimtuhumu kuwa ni Teleza na wakidai kwamba ndiye anaye wabaka na kulawiti wanawake wa maeneo hayo. 

“Taarifa hizo si za kweli,bali ni zakufikirika na kutokana na kitendo hicho,hatutasitakuchukua hatua za kisheria kwa wataobainika kuhusika kutenda uhalifu huo, ikiwemo wanaochapisha na kutoa taarifa potofu kwa wananchi kwani zinaweza kuleta taharuki na uvunjifu wa amani,”amesema Mutafungwa.

Hata hivyo ametoa wito kwa  wananchi wenye taarifa yoyote ya uhalifu au viashiria vya uvunjifu wa amani watoe taarifa kwa jeshi la polisi ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa.