February 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madereva 16,Mwanza wafungiwa leseni ya udereva

Judith Ferdinand,Timesmajira Online,Mwanza

 Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza katika kipindi cha Desemba 1 hadi 30,2024,limewafungia  madereva 16,leseni za udereva  kwa muda wa miezi sita.

Ikiwa ni ongezeko la madereva 10,ikilinganishwa na kipindi cha  Desemba 1 hadi 31,2023,ambapo madereva 6,walifungiwa leseni za udereva.

Akizungumza  Desemba 30,2024,mkoani hapa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP.Wilbrod Mutafungwa,amesema,baada ya miezi hiyo sita kuisha madereva hao watapaswa kusomea tena udereva katika vyuo vinavyotambulika na kisha kurudi polisi ili wajaribiwe kama wameiva ili waweze kupata leseni upya.

Pia Mutafungwa,amesema katika kipindi cha Desemba 1 hadi 30,2024,jumla ya magari 17,ya kubeba abiria yalizuiliwa  yasiendelee na safari,baada ya kukaguliwa na kubainika kuwa na ubovu.Mpaka wamiliki walipoyarekebisha na kukaguliwa ndipo yaliruhusiwa kuendelea na safari,lengo likiwa ni kulinda usalama wa wananchi.

Sanjari na hayo,amesema katika kipindi cha Desemba 1 hadi 30,2024,wamefanikiwa kupunguza uhalifu kwa asilimia 13,kupitia doria na misako inayoendelea,walifanikiwa  kukamata makosa 2,525 na watuhumiwa 3,510 wa makosa ya jinai huku makosa hatarishi ya usalama barabarani 15,307 na watuhumiwa 14,851.

Ambapo ikilinganishwa na  kipindi kama hicho cha  Desemba 1 hadi 31,2023,makosa ya jinai yalikuwa 1,820  na  watuhumiwa wa makosa ya jinai 2,215,huku watuhumiwa 13,320,wa makosa hatarishi ya  usalama barabarani walikamatwa.

“Sawa na ongezeko ya la watuhumiwa wa makosa ya jinai 1,295   na watuhumiwa 1,522,wa makosa hatarishi ya usalama barabarani.Watuhumiwa wa makosa ya jinai kwa mwaka huu wamekamatwa  kwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu,kupatikana na mali zinazodhaniwa  kuwa za wizi,kucheza Kamari,wizi,mauaji,ubakaji,ulawiti pamoja na kujihusisha na vitendo vya ukahaba,”amesema Mutafungwa.

Aidha,amesema,ongezeko hilo la makosa na watuhumiwa kukamatwa,linatokana na jitihada zinazofanywa na jeshi hilo mkoani kutokana na kuimarisha mifumo ya kiusalama  pamoja na ushirikiano wa wananchi wanaoutoa kwa polisi.