January 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watano wa familia moja wafariki kwa radi Chunya

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

WATOTO watano wa familia Katika  kitongoji cha Nkangi kata ya Matwiga Wilaya ya Chunya mkoa wa Mbeya wamefariki dunia baada ya kupigwa na radi wakati wakiwa wamelala kwenye kambi ya kuchungia ng’ombe kijijini hapo.

Akizungumza na waandishi wa habari Disemba 29,2024  Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya,Benjamin Kuzaga amesema tukio hilo limetokea majira ya saa 8:30 usiku katika Kitongoji cha Nkangi kilichopo Kijiji cha Isangawana, Kata ya Matwiga, Tarafa ya Kipembawe, Wilaya ya Chunya.

Aidha Kamanda kuzaga amewataja waliofariki katika tukio hilo kuwa  ni Balaa Scania(28),Kulwa Luweja(17),Masele Masaganya(16),Hema Tati(10) na Manangu Ngwisu (18)wote wakazi wa Kijiji cha Nkangi.

Hata hivyo  Kuzaga amesema kuwa  katika tukio hilo watu wengine watano walijeruhiwa ambao ni Gulu Scania (30), Manyenge Masaganya(13),Seni Solo(13), Paskali Kalezi(16)na Huzuni Kalezi(19) wote wakazi wa Kijiji cha Nkangi.

Akielezea zaidi Chanzo cha tukio Kamanda Kuzaga amesema ni mvua kubwa iliyonyesha usiku ikiambatana na radi hivyo kusababisha vifo vya watu watano na wengine watano kujeruhiwa.

Kuzaga ameeleza kuwa Majeruhi  walikimbizwa katika Kituo cha Afya Isangawana kwa matibabu na kutibiwa  na kuruhusiwa kwenda nyumbani baada ya hali zao kuwa nzuri.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa jamii kuchukua tahadhari kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha kwa kuepuka kukaa karibu na miti mikubwa.

“Kwa mvua hizi za kipindi hiki ni vema kuchukua tahadhari kwa maeneo yote hususani vijijini ili kuweza kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza “amesema Kamanda Kuzaga.