Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Magu
Katika kipindi cha miaka minne ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM),Jimbo la Magu mkoani Mwanza,limepokea kiasi cha bilioni 143.9, kutoka serikalini wa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo jimboni humo.
Hayo yamebainishwa Desemba 23,2024, na Mbunge wa Jimbo la Magu,Boniventura Kiswaga,wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha 2020-2024.
Mfuko wa Jimbo
Kiswaga amesema katika kipindi hicho,zaidi ya milioni 336.7, zilipokelewa na Mfuko wa kuchochea maendeleo ya Jimbo.Ambapo jumla ya miradi 52, ilichochewa na Mfuko huo kati yake miradi 28 ni ya afya,20 ya elimu,3 ni utawala huku mmoja ni wa barabara.
Sekta ya barabara
Amesema katika kipindi hicho Jimbo la Magu lilipokea zaidi ya bilioni 78.8, kwa ajili ya kutekeleza miradi ya barabara.
Kati ya fedha hizo bilioni 7.1,zilipokelewa na Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini(TARURA),Magu,kwa ajili ya kuhudumia barabara za Jimbo la Magu,ambapo jumla ya Kilomita 1524.15 za mtandao wa barabara zimeendelea kufanyiwa matengenezo kutokana na mahitaji na fedha kutoka serikalini.
Sekta ya usafiri majini
Kiswaga amesema,bilioni 5.3, zinagharimu ujenzi wa kivuko cha Ijinga-Kahangara,ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 89.9,ambacho kikikamilika kitafungua fursa za uchumi kwa wananchi wa Kisiwa cha Ijinga.
Sekta ya Maji
Amesema,katika kipindi hicho cha 2020-2024,Jimbo la Magu lilipokea zaidi ya bilioni 12.1, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji,kati ya fedha hizo bilioni 3.5, zinatumika kwa ajili ya ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji la Bujora-Kisesa lenye uwezo wa lita za maji milioni 5,ambao umefikia asilimia 93 ya utekelezaji wake na unatarajiwa kukamilika Februari ,2025.
“Baada ya kukamilika kwa mradi mpya wa maji Magu mjini,unaendeshwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza(MWAUWASA),wenye uwezo wa kuzalisha na kutibu maji lita za ujazo milioni 7.25 kwa siku, idadi ya watumishi maji umeongezeka toka asilimia 92.5,mwaka 2020 hadi asilimia 93.3, mwaka 2024,”amesema Kiswaga na kuongeza:
“Hadi sasa jumla ya watu 68,694 kati ya 73,600,wanahudumiwa na mradi huo katika Kata za Itumbili,Magu Mjini,Isandula,Kandawe,Nyigogo, na baadhi ya maeneo ya Kata ya Kahangara.Huku mtandao mpya wa maji qa kilomita 41.25,zimejengwa kwa gharama ya zaidi ya milioni 270,”.
Pia amesema,kwa upande wa maji vijijini,Wakala wa Maji na usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA),imeweza kutekeleza ujenzi,usimamizi na ukamilishaji wa jumla ya miradi 18, yenye thamani ya zaidi ya bilioni 8.3.
Huku ongezeko la watumishi maji vijijini kutoka asilimia 56, mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 75, mwaka 2024, jimboni humo ikiwa ni ongezeko la asilimia 19.
“Miradi inaendelea kutekeleza kwenye baadhi ya maeneo ikiwemo Sagani-Mwamabanza,Iseni-Nyang’hanga, Misungwi -Lumeji,ikikamilika itapunguza kwa kiwango kikubwa uhaba wa maji safi na salama vijijini,”.
Sekta ya Elimu
Amesema zaidi ya bilioni 31,zilipokelewa jimboni Magu, na kutekeleza miradi ya elimu ya awali,msingi, sekondari na vyuo vya ufundi.Ambapo Jimbo hilo limefanikiwa kupata vyuo viwili ya ufundi stadi,kimoja kinajengwa kijiji cha Nsola cha VETA Wilaya ya Magu,chenye thamani ya bilioni 1.6 huku ujenzi wake ukiwa umefikia asilimia 60, na kinatarajia kukamilika Februari 2025.
Huku chuo kwa ajili ya watu wenye ulemavu limejengwa Kanyama wilayani Magu kwa gharama ya milioni 600.
Hata hivyo katika kipindi cha Januari,2021 hadi Juni 2024, Halmashauri ya Magu, imetekeleza miradi ya zaidi ya bilioni 21 ya elimu sekondari ikiwa ni pamoja na ujenzi na usajili wa shule mpya za sekondari 19, ikiwemo ya Wasichana Mwanza(Mwanza Girls).Huku shule 17, zikiendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali.
Ukamilishaji wa vyumba vya madarasa 109, ujenzi wa vyumba vya madarasa 336,ujenzi wa nyumba 7 za walimu, ujenzi wa vyumba 15, vya maabara,ujenzi wa matundu ya vyoo 228 katika shule mbalimbali za sekondari.
Pia amesema,elimu msingi katika kipindi cha Januari,2021 hadi Juni,2024, Halmashauri ya Magu, imetekeleza miradi yenye thamani ya zaidi ya bilioni 7.3, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule mpya ya msingi ya Chifu Hangaya, ujenzi wa vyumba vya madarasa 25, katika shule za msingi Nyalikungu, Igombe na Isangijo.
Pia ujenzi wa vyumba vya madarasa 67, ukamilishaji wa vyumba vya madarasa 84, ujenzi wa nyumba 9, za wà limu pamoja na ujenzi wa matundu ya vyoo 149, katika shule za msingi mbalimbali.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato