Na George Mwigulu,Timesmajiraonline, Katavi.
SERIKALI Mkoa wa Katavi imesema kwa miaka mitatu na nusu kiasi cha fedha Trioni 1.3 zimebadilisha maisha ya wananchi kuwa bora kupitia ujenzi miradi ya maendeleo.
Miradi hiyo ni ujenzi wa miradi ya maendeleo katika sekta ya uchukuzi, afya, umeme, elimu, maji sanjali na ujenzi wa miundombinu ya kilimo na mbolea za ruzuku umemgusa mwananchi wa kawaida kuweza kujikwamua kiuchumi.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko, Katika ripoti aliyoitoa Disemba 21,2024 ameweka wazi kuwa fedha hizo kupelekwa kwenye sekta mbalimbali zimefanikisha kutatua kero za wananchi.
Akiwa katika ukumbi wa Manispaa ya Mpanda Social Hall kwenye Kikao cha halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) cha mkoa huo amekiambia kuwa usimamizi bora wa miradi unatokana na uadilifu wa watendaji.
Katika kipindi cha mwezi Julai, 2023 hadi Septemba 2024 ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami yenye urefu wa Km 112 kutoka Mpanda kwenda bandari ya Karema iliyogharimu fedha Bil 48 umeanza kufanyika.
Ujenzi wa barabara hiyo unatarajia kuwezesha bandari ya Karema kufanya kazi kwa ufanisi kuliko ilivyo sasa kwani utasaidia kusafirisha mizigo mbalimbali kwa kipindi chote.
Mrindoko amesema sekta ya kilimo wamefanikiwa kuvuna tani milioni 1.43 za mazao ya chakula na biashara kwa msimu wa mwaka 2023/2024 huku matarajio kwa msimu wa mwaka 2024/2025 ni kuvuna zaidi ya tani Milioni 1.4 yote ni kwa sababu ya serikali kutoa kwa wakulima mbolea ya ruzuku.
“Serikali imeleta zaidi ya tani milioni 6 za mbolea za ruzuku kwa wakulima zenye thamani ya fedha bilioni 4.5 huku fedha bilioni 31.7 zinajenga mradi wa umwagiliaji kata ya Mwamkuru na fedha bilioni 23.8 mradi wa umwagiliaji wa Kabage haya ni mafanikio makubwa” Amesema.
Kiongozi huyo wa Mkoa, Amefafanua sekta za jamii za afya na elimu serikali imefanikiwa kujenga shule 129 kati ya hizo shule 97 ni za msingi na sekondari ni 32.
Vilevile amesema hivi sasa wanaendelea na ujenzi wa shule zingine tisa ambapo shule moja itakuwa maalumu ya wavulana inayojengwa katika manispaa ya Mpanda.
Amefafanua ujenzi wa hosptali ya rufaa ya mkoa wa Katavi ambayo inaendelea na utoaji huduma za afya kwa wananchi, Serikali tayari imetoa fedha zingine za ujenzi wa awamu ya pili huku vifaa tiba vikiendelea kutolewa na idadi ya magari ya wagonjwa yakiongezeka kutoka 10 hadi 16.
Sekta ya maji imeimarishwa ambapo kunaongezeko la upatikanaji wa maji safi na salama na kufikia asilimia 76.7 huku miradi mingine ya maji ikiendelea kujengwa kama vile mradi wa miji 28 Mpanda wenye thamani ya fedha bilioni 28.
Meneja wa Wakala wa barabara TANROADS Mkoa wa Katavi Mhandisi, Martin Mwakabende amesema kwa mwaka wa fedha 2024/2025 wamepokea kiasi cha fedha bilioni 15 kwa ajii ya matengenezo ya barabara.
Aidha fedha bilioni 17.6 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa madaraja matatu ya Sitalike na Mirumba na tayari wakandarasi wameanza kazi.
Mbunge wa Jimbo la Nsimbo Anna Lupembe amesema kuwa fedha zote zilizotolewa na serikali katika majimbo yote ya mkoa wa Katavi zinalenga kumkwamua mwananchi kiuchumi kwa kumtengenezea mazingira rafiki ya kufanya kazi.
Lupembe licha ya kumpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri amewaomba wananchi kuendelea kutumia fursa zilizopo mkoani humo kwa kufanya kazi kwa nguvu zote.
More Stories
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam
MSF ilivyojidhatiti kusaidia serikali katika utoaji wa huduma za afya