Na Suleiman Abeid,Majira Online, Shinyanga.
MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Manispaa ya Shinyanga (SHUWASA),inatarajia kutumia zaidi ya milioni 300,kwa ajili ya kuongeza mtambo wa kuchakata tope kinyesi kinachosombwa kutoka Mji wa Shinyanga na kufikia uwezo wa kuchakata mita za ujazo 100 kwa siku.
Mtambo uliopo kwa hivi sasa una uwezo wa kuchakata tope kinyesi mita za ujazo 40 kwa siku na tayari ukarabati huo, umefikia asilimia 62 na kukamilika kwake kunatarajiwa kunufaisha wakazi wapatao laki mbili katika Manispaa ya Shinyanga na Miji jirani.
Kwa mujibu wa taarifa ambayo imetolewa na Meneja Uendeshaji Miundombinu ya SHUWASA, Mhandisi Wilfrred Lameck,lengo la ukarabati huo ni kuongeza utoaji huduma kwa wakazi wa Manispaa ya Shinyanga na kuwezesha mji kuwa katika hali ya usafi wakati wote.
“Ukarabati huu umelenga kuongeza utoaji huduma wa SHUWASA kwa wakazi wa Manispaa ya Shinyanga,tunarajia utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuchakata taka kinyesi kwa mita ujazo 100 kwa siku badala ya 60 za hivi sasa,” ameeleza Mhandisi Lameck.
Mhandisi Lameck amesema adhima ya kuongeza uwezo wa mtambo huo inatokana na mwitikio wa wananchi, kuondosha taka kinyesi kwa kutumia magari tofauti na siku za nyuma ambapo wengi wao walikuwa wakitumia mfumo wa kutapisha na kufukia chini taka kinyesi jambo ambalo lilikuwa na madhara upande wa kiafya.
Amefafanua kwa kusema kwamba kazi hiyo ya ukarabati ambayo ni awamu ya pili inatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Februari hapo mwakani ambapo mkandarasi atakuwa amekamilisha kazi hiyo na kuikabidhi rasmi hivyo changamoto ya kuzidiwa kwa mtambo uliopo hivi sasa.
Mkandarasi Swalehe Maganga kutoka kampuni ya Kanuta Engineering Supply, amesema anaamini iwapo mipango itakwenda kama walivyoipanga kazi ya ukarabati huo itakamilika ndani ya muda uliopangwa kwenye mkataba wa utekelezaji wa kazi hiyo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola, amesema fedha zinazotumika kukarabati mradi huo zinatokana na mkopo kiasi cha shilingi milioni 735 kutoka Benki NMB kutokana na maelekezo ambayo yametolewa na Bodi ya Wakurugenzi.
“Mbali ya mradi huu tunataraji kuwa na mradi mwingine wa kusambaza majitaka ambao utakuwa na sehemu mbili moja ni kwenye eneo la viwanda na baadhi ya maeneo ya kata za Mjini, Ngokolo, Kambarage na Lubaga, kata hizi zitakuwa na mtando maalum ambao mtambo wake utakaojengwa kule eneo la Mwagala,” ameeleza Mhandisi Katopola.
Akifafanua Mhandisi huyo amesema kwa sasa mtambo uliopo eneo la Nhelegani unachakata taka kinyesi zinazotoka maeneo ya wakazi wa mji wa Shinyanga na kwamba mradi wa usambazaji majitaka utawezesha pia kuhudumia eneo la viwanda vilivyopo katika Manispaa ya Shinyanga.
More Stories
MSF ilivyojidhatiti kusaidia serikali katika utoaji wa huduma za afya
Prof.Muhongo awapongeza vijana 32 waliotembea kwa miguu kutoka Butiama hadi Mwanza
Rais Samia atimiza ahadi Hanang