Judith Ferdinand,Timesmajira Online,Mwanza
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,amemtaka Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza(MWAUWASA),Neli Msuya,kutekeleza ahadi yake ya kufikia Februari 15,2025, mradi wa ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji la Bujora- Kisesa,uwe umekamilika na wananchi wa maeneo hayo wawe wameanza kupata huduma ya maji.
Utekelezaji wa mradi huo ambao umefikia asilimia 93,wenye thamani ya bilioni 3.5,unatarajia kunufaisha wananchi takribani 75.000,wa maeneo ya Bujora,Kisesa na maeneo ya jirani.
Majaliwa amesema hayo,Desemba 21,2024,wakati alipotembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo Wilaya ya Magu ikiwemo ya ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji Bujora-Kisesa,ambalo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi lita za maji milioni 5.
Amesema,asilimia 7,zilizobaki ili mradi huo kukamilika Kaimu Mkurugenzi huyo asimamie na uwe tayari kama alivyoahidi kuwa kufikia Februari utakuwa umekamilika, kwani wananchi wa maeneo hayo wanasubili maji kutoka katika tenki hilo.
“Kwa hatua hii,najua maji yatakuja,Februari 2025,Mwenyezi Mungu akitujalia kuvuka nitakuja , nikute maji yameanza kutoka kwa wananchi wa Bujora,Kisesa na maeneo mengine,”amesema Majaliwa.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa MWAUWASA,Neli Msuya,amesema,mradi wa ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji Bujora-Kisesa,ni moja ya mradi wa kimkakati wa kuboresha huduma ya maji katika maeneo ambayo yalikuwa yanakabiliwa na changamoto ya maji ndani ya Mkoa wa Mwanza.
Ambapo amesema,mpango wa kuboresha huduma ya hupatikanaji maji jijini Mwanza,Serikali imetoa kiasi cha bilioni 49 kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa matenki matano yenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni 31 likiwemo hilo la Kisesa lenye uwezo wa lita milioni 5.Ambayo utekelezaji wake unatarajia kukamilika Desemba,2026.
Matenki mengine yatajengwa maeneo ya Nyamazobe tenki lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni 10,Buhongwa tenki lenye uwezo lita milioni tano za maji ,Fumagaila lita milioni 10 na Usagara lita milioni moja.
“Mradi wa ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji Bujora-Kisesa,Mkandarasi amepewa maelekezo mahususi yakuanza kazi ya kulaza mabomba kutoka kwenye kituo cha Sahwa hadi kwenye tenki hilo.Mradi huu una thamani ya bilioni 3.5,ulianza Juni 2023 na unatarajia kukamilika Februari 15,2025,na mpaka sasa Mkandarasi ameishalipwa kiasi cha bilioni 2.9,”ameeleza Neli.
Naye Waziri wa Maji,Jumaa Aweso,amesema Rais Samia Suluhu Hassan,ataki kuona wanawake wanateseka na maji,hivyo ameunga mkono Wizara hiyo kwa kuipatia fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maji ikiwemo bilioni 3.5,kwa ajili ya ujenzi wa tenki hilo la kuhifadhia maji la Bujora –Kisesa,ili kuwaondolea adha ya ukosefu wa maji wananchi wa maeneo hayo.
Mbunge wa Jimbo la Magu Boniventure Kiswaga,amesema Serikali imeipatia Wilaya ya Magu kiasi cha bilioni 12 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji, kati ya fedha hizo bilioni 3.5,zinatekeleza mradi wa ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji la Bujora-Kisesa.
“Tunaipongeza Serikali kupitia miradi ya maji ya matokeo ya haraka, kwani wakazi wa Kisesa na Bujora walikuwa na hali mbaya,ukisimama watu walikuwa wanasema maji, lakini sasa kuna unafuu,”amesema Kiswaga.
More Stories
Prof.Muhongo awapongeza vijana 32 waliotembea kwa miguu kutoka Butiama hadi Mwanza
Rais Samia atimiza ahadi Hanang
Daktari Dar ajishindia Mil. 100/- za Fainali NMB Bonge la Mpango