Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online DSM
BODI ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imeidhinisha matokeo ya mitihani ya 100 ya bodi hiyo iliyofanyika Novemba, 2024 ambapo ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 66.4 kwa mwaka uliyopita na kufikia asilimia 70.3, huku wanaume wakiongoza kwa ufaulu.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) CPA. Pius Maneno imeeleza kuwa watahiniwa waliofanya mitihani hiyo walikuwa 6,908 sawa na asilimia 91.3 kati yao wanaume walikuwa 3,802 na wanawake walikuwa 3,764 huku watahiniwa 658 sawa na asilimia 8.7 hawakufanya mitihani kwa sababu mbalimbali.
Aidha, amesema kati ya watahiniwa 6,908 waliyofanya mitihani hiyo, watahiniwa 4,858 sawa na asilimia 70.3 wamefaulu mitihani yao ambapo watahiniwa 1,282 sawa na asilimia 18.6 wamefaulu masomo yote katika ngazi husika, hivyo wamestahili kupatiwa barua za ufaulu.
“Watahiniwa wengine 3,576 sawa na asilimia 51.7 wamefaulu baadhi ya masomo katika ngazi husika na watahiniwa 2,050 waliobaki sawa na asilimia 29.7 hawakufaulu mitihani yao.
“Bodi ya NBAA, inawapongeza wale wote waliofuzu mitihani yao na kuwataka wale ambao hawajafuzu kutokata tamaa bali waongeze bidii zaidi katika masomo yao ili waweze kufanya vizuri katika mitihani ijayo ya bodi,”amesema.
Aidha amesema bodi inawashauri kuendelea kutumia vema vitabu vilivyotayarishwa na bodi katika kujiandaa kwa mitihani yao kwa kusoma vitabu vingine vya ziada ili kuongeza ufahamu zaidi katika masomo hayo.
More Stories
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais
NIDA yawakumbusha wananchi kuchukua vitambulisho vyao