Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
VYAMA vya Ushirika wa Akiba na Mikopo barani Afrika vimetakiwa kujizatiti kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii yenye matokeo yanayopimika kwa wananchi, badala ya kuishia katika kauli na maazimio ya mikutano.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, wakati wa kuhitimisha Kongamano la 26 la Kimataifa la Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo Barani Afrika (SACCA Congress 2026), lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Kombo amesema mafanikio ya kongamano hilo hayapaswi kupimwa kwa idadi ya hotuba zilizotolewa au maneno yaliyosemwa, bali kwa maisha yaliyoboreshwa, biashara zilizopata mitaji, ajira zilizozalishwa na jamii zilizopiga hatua za maendeleo.

Amesema ni muhimu kwa taasisi hizo kuandaa mpango mahsusi wa utekelezaji wa maazimio ya kongamano hilo, ukiainisha vipaumbele, majukumu ya kila taasisi na malengo yanayopimika ili kurahisisha ufuatiliaji wa maendeleo yatakayofikiwa.
“Ujumbe wangu kwenu ni kwamba mkutano wa Dar es Salaam usikumbukwe tu kama mahali tulipokutana, bali kama mahali tulipojizatiti kuleta mabadiliko na matokeo yanayopimika,” amesema Kombo.

Amezitaka taasisi hizo kurejea katika nchi zao zikiwa na dhamira mpya ya kuimarisha utawala bora, kuharakisha mabadiliko ya kidijitali yanayowajibika na kupanua fursa za kiuchumi kwa wanawake na vijana.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuelekeza rasilimali za vyama vya ushirika katika sekta za uzalishaji, zikiwemo kilimo, uvuvi na ufugaji, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuchochea shughuli za kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Kombo amesema vyama hivyo vina wajibu wa kulinda akiba na maslahi ya wanachama huku vikiimarisha ushirikiano wa vitendo kati ya taasisi za ushirika barani Afrika.

Ameeleza kuwa Afrika ina rasilimali watu, vipaji na fursa nyingi za kiuchumi, lakini inahitaji kujenga taasisi imara, kuimarisha ushirikiano na kukuza uaminifu ili kutumia fursa hizo kuleta ustawi kwa wananchi.
“Tusilenge tu kukusanya akiba, bali tutengeneze fursa; tusilenge tu kuimarisha taasisi, bali tuboreshe maisha ya watu wetu,” amesema.
Amesisitiza kuwa maendeleo ya Afrika yanahitaji zaidi ya kauli na mipango, yakihitaji uwekezaji wa rasilimali fedha na ushirikiano wa pamoja ili kuhakikisha wananchi wananufaika na fursa zilizopo.
Amewataka wadau wa ushirika barani Afrika kuendeleza mshikamano na kuelekeza nguvu zao katika utekelezaji wa maazimio ya kongamano hilo ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika bara hilo.

More Stories
Ndejembi akerwa na udanganyifu TANROADS Mbeya
QNET yakanusha kuwalaghai vijana 125 Singida
Samizi:Uchunguzi wa mapema wa saratani ya matiti huokoa maisha