December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kapinga atangaza fursa za uwekezaji nchini Saud Arabia

๐Ÿ“ŒAshiriki kongamano la wafanyabiashara na wawekezaji nchini humo

๐Ÿ“Œ Zaidi ya wafanyabiasha,wawekezaji 250 wakutana

๐Ÿ“Œ JNHPP yatajwa kuongeza uhakika wa uwepo wa umeme

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Saudi Arabia

Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga amesema kongamano la wafanyabiashara na wawekezaji nchini Saudi Arabia, litaongeza uwekezaji kwenye sekta ya nishati kutokana na Tanzania kuzinadi fursa zilizopo kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo gesi asilia,umeme na nishati safi ya kupikia.

Kapinga amesema hayo katika kongamano la wafanyabiashara na wawekezaji zaidi ya 250 kutoka Tanzania na Saudi Arabia linalofanyika,Desemba 18 na 19,2024 katika Mji wa Riyadh nchini Saudi Arabia.

Amesema kuwa,kongamano hilo ni muhimu kwa upande wa Wizara ya Nishati na nchi kwa ujumla, kwani linatangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini kupitia sekta ya nishati.Ambapo kwa sasa Tanzania ina vyanzo vingi vya kuzalisha umeme mwingi na wa uhakika likiwemo Bwawa la Julius Nyerere ambalo litazalisha jumla ya megawati 2,115.

” Kongamano hili litaendelea pia kujenga uhusiano kati ya Tanzania na wadau kutoka Saudi Arabia katika sekta ya nishati,” amesema Kapinga.

Akifungua kongamano hilo,Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo,amewakaribisha wawekezaji kuja nchini Tanzania kwani kuna fursa nyingi za uwekezaji, kupitia sera nzuri,misingi imara na rafiki iliyowekwa.

Amesema maeneo ya uwekezaji nchini ni pamoja na nshati,madini,viwanda,biashara, kilimo,miundombinu pamoja na uchumi wa buluu.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Dkt. Mahโ€™d Juma Abdalla,amewaasa watanzania wanaoshiriki katika kongamano hilo, kutumia fursa hiyo kuitangaza vyema nchi yao na kutanua wigo wa biashara zao,kwani nafasi kama hizo ni aghalabu kupatikana.

Mawaziri mbalimbali waliohudhuria kongamano hilo ni Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jaffo, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Madini, Antony Mavunde na Naibu Waziri wa nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Ajira na Uwekezaji Zanzibar, Sharif Ali Sharif.

Viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi zake wanaoshiriki Kongamano hilo ni Kamishna Msaidizi wa Petroli, Mhandisi Joyce Kisamo, Mkurugenzi Msaidizi wa Sera, Utafiti na Ubunifu, Oscar Kashaigiri na Meneja wa Biashara ya Mafuta wa kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Baraka Nyakutonya.