Na Penina Malundo,Timesmajira
Wasanii wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupima afya zao wakati wa kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo itakayofanyika hivi karibuni katika Kliniki ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Kawe.
Rai hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma ya upimaji na matibabu ya moyo bila malipo itakayotolewa kwa wasanii.
Dkt. Kisenge amesema kutokana na tatizo la magonjwa ya moyo kuwa kubwa Taasisi hiyo imeona ishirikiane na wasanii katika kuhamasisha jamii ili kuona umuhimu wa kupima magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo.
“Upimaji huu wa magonjwa ya moyo utafanyika bila malipo kwa wasanii katika kliniki yetu ya Kawe kwa mwezi huu wa Desemba na Januari 2024 kila siku za Jumamosi na Jumapili”,amesema .
Amesema zoezi hilo litakapokamilika wataandaa zoezi la utaratibu maalum kwa wasanii ambao hawana bima za afya watakaokuja kutibiwa katika kliniki yao watakuwa wanapata punguzo la gharama za matibabu.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Dkt. Kedmon Mapana ameishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuona umuhimu wa kupima afya za mioyo ya wasanii na kuwapa elimu ya jinsi ya kujiepusha na magonjwa hayo bila ya gharama zozote zile.
“BASATA tutasimamia zoezi hili la upimaji kwa wasanii wetu ili kila mmoja anufaike na upimaji huu kama mlivyosikia gharama za matibabu ya magonjwa ya moyo ni kubwa hivyo basi ni muhimu mkachukuwa hatua za kupima mapema kabla ya kusubiri kuugua”, amesema Dkt. Mapana.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao Steven Mongele ambaye ni Mratibu wa zoezi hilo la upimaji ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza katika tiba ya moyo nchini jambo linalowafanya wananchi wakiwemo wasanii kufaidika na huduma za matibabu ya kibingwa.
“Gharama za matibabu ya kibingwa yakiwemo ya moyo ni kubwa lakini hivi sasa huduma hizi zinapatikana hapa nchini na hakuna haja ya kupeka wagonjwa nje ya nchi. Jambo la muhimu ni kupima afya zetu mapema na kama utajigundua unashida utajua jinsi gani utaishi pia tujenge tabia ya kusaidiana tunapoona wenzetu wanahitai msaada wa fedha za matibabu”, amesema Mongele.
Aidha amesema wataangalia namna ambavyo wasanii walioko mikoani watafikiwa na huduma hiyo ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo bila malipo.
More Stories
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam
MSF ilivyojidhatiti kusaidia serikali katika utoaji wa huduma za afya
Prof.Muhongo awapongeza vijana 32 waliotembea kwa miguu kutoka Butiama hadi Mwanza