December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yandelea kuweka mikakati ya kuboresha huduma za afya

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mikakati ya kuboresha huduma za afya, hususan huduma za dharura ambapo imeweka mikakati ya kina kwa ajili ya kujenga uwezo wa mfumo wa afya, ikiwa ni pamoja na kuidhinisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.

Hatua hizo zinalenga kuhakikisha kwamba huduma za dharura zinapatikana kwa urahisi, zenye ubora, na zinakidhi mahitaji ya wananchi kwa wakati.

Hayo yalisemwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Mohamed Manguna wakati akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila katika hafla rasmi ya kufunga awamu ya kwanza ya mradi wa kuboresha huduma za dharura za Afya Tanzania (IMECT) uliofanyika kwa ushirikiano wa taasisi za umma na binafsi unaofadhiliwa na serikali ya Poland kupitia kituo cha msaada wa kimataifa cha Poland kwa kushirikiana na Taasisi ya Huduma za Afya za Aga Khan Tanzania pamoja na serikali ya Tanzania.

Alisema Mradi huo wa IMECT wenye thamani ya TZS Bilioni 1.8 ni mfano bora wa mafanikio ya ushirikiano, ukileta pamoja Serikali ya Tanzania, washirika wa kimataifa, na jamii za ndani katika jitihada za kuimarisha huduma za matibabu ya dharura kote nchini.

“Mradi wa IMECT ni mfano bora wa mafanikio ya ushirikiano, ukileta pamoja Serikali ya Tanzania, washirika wa kimataifa, na jamii za ndani katika jitihada za kuimarisha huduma za matibabu ya dharura kote nchini.
Natumia fursa hii kuishukuru Serikali ya Poland kupitia Kituo cha Msaada wa Kimataifa cha Poland (PCPM) na Huduma za Afya Aga Khan Tanzania (AKHST) kwa hatua kubwa waliyopiga ya kutambua hitaji na kutoa ufadhili wa kiasi cha dola za Marekani 760,000, sawa na shilingi za Kitanzania bilioni 1.8, kwa lengo la kuboresha huduma za dharura nchini katika kipindi cha miaka miwili na nusu iliyopita.”

Aliongeza kuwa Njia ya kuboresha huduma za dharura Tanzania inaendelea, na kupitia ushirikiano huo, wataweza kubadilisha mandhari ya huduma za dharura nchini Tanzania.

Pia alipongeza huduma za Afya za Aga Khan Tanzania kwakuwa ni mfano wa kuigwa katika ushirikiano wa sekta ya Umma na Binafsi kwa juhudi zake za kusaidia juhudi za serikali katika kuimarisha mifumo ya afya.

“Ingawa Serikali imeanza kuchukua hatua za Kutambua zaidi eneo hili na kuhakikisha kila kituo cha afya kina maarifa, ujuzi, miundombinu, na vifaa vinavyohitajika kutoa huduma bora za dharura kwa hali za dharura na ajali; bado kuna upungufu wa rasilimali na ujuzi wa kutuwezesha kufanikisha kikamilifu. Kwa hivyo, Taasisi ya Huduma za Afya ya Aga Khan, kwa kushirikiana na Kituo cha Msaada wa Kimataifa cha Poland na Serikali ya Tanzania, kupitia mradi huu wamekuja na mpango wa kuboresha huduma za harura na wameleta tofauti kubwa.”

Kwa upande wake Waziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya Poland Jakub Wisniewski alisema wanafuraha kushirikiana na serikali ya Tanzania kupitia Taasisi ya Huduma za afya ili kuimarisha huduma hizo za dharura

“Tunafurahi na tunajivunia kushirikiana na serikali ya Tanzania kupitia Taasisi ya huduma za Afya za Aga Khan ili kuimarisha huduma za dharura , kwakuwa hii ilikuwa ni mara ya kwanza Poland kuwekeza katika sekta ya afya nchini Tanzania na kwa matokeo mazuri kama haya ni mwanzo wa uwezekano wa ushirikiano zaidi siku zijazo”

Naye Mratibu wa Huduma za Dharura na Utunzaji Muhimu kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Erasto Sylvanus, aliishukuru timu za usimamizi wa vituo vyote vilivyoshirikiana kwa uongozi na msaada wao wakati wa utekelezaji wa mradi.

“Naipongeza Serikali ya Tanzania, kupitia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuunga mkono ushirikiano wa sekta nyingi kati ya umma na binafsi ili kushughulikia mahitaji ya jamii na mifumo ya afya.”

Dkt. Hussein K. Manji, Mratibu wa Mradi, Taasisi ya Huduma za Afya ya Aga Khan Tanzania alisema: “Fani ya Magonjwa za Dharura ni taaluma maalum yenyewe, na haitoshi tu kujua la kufanya, bali pia kuwa na rasilimali na uwezo wa kutumia ujuzi huo kwa vitendo ni muhimu. Tunapojenga uwezo na kuimarisha miundombinu, tunalenga kupunguza rufaa,
kupunguza vifo, na kuwapa wananchi wetu walioko katika hali mbaya nafasi bora zaidi ya kupona.”