December 12, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

GST,BGS zafanya majadiliano namna ya kuanzisha mashirikiano katika tafiti na kujengeana uwezo

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Taasisi ya Jiolojia ya nchini Uingereza (BGS) zimefanya mazungumzo ya namna bora ya kuanzisha mashirikiano katika tafiti za madini na kujengeana uwezo.

Taasisi hiyo ya Jiolojia kutoka nchini Uingereza ikuwa na GST kwa muda wa siku 3 kwa lengo la kujifunzo namna GST inavyotekeleza majukumu yake kwa kufanya ziara ya kujifunza katika Kurugenzi ya Huduma za Jiolojia, Kanzidata na Maabara.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha, Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba amewashukuru wataalamu hao kutoka BGS kwa kuona umuhimu wa kuanzisha mashirikiano na GST na kuahidi kutoa ushirikiano katika kufikia lengo lililokusudiwa.

Amefafanua kuwa, ushirikiano huo umelenga katika matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kutafiti madini ya kimkakati, kuratibu majanga ya asili ya jiolojia pamoja na kujengeana uwezo kwa kubadilishana uzoefu.

Katika hatua nyingine, Dkt. Budeba amewazawadia watalaamu hao wa BGS toleo jipya la kitabu cha madini viwanda kama sehemu ya kuvutia uwekezaji mkubwa katika madini viwanda ambapo miongoni mwao yamo madini ya kimkakati.