Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline, Dar
SHIRIKISHO la Wenye Viwanda nchini (CTI), limesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inastahili kupewa maua yake kwa namna inavyosikiliza na kutatua changamoto mbalimbali za wafanyabiahara zikiwemo za kikodi zilizokuwa sumbufu.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Shirikisho hilo, Ledegar Tenga, wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu uliofanyika jijini Dar es Salaam.
“CTI itaendelea kufanyakazi kwa karibu na Serikali kufanikisha maendeleo ya viwanda ili kukuza uchumi na kwenda sawa na azma ya serikali ya awamu ya sita ya kujenga uchumi wa viwanda,” alisema
Kuhusu changamoto za wenye viwanda, Tenga alisema changamoto za wenye viwanda ni zile zile na Serikali imefanya jitihada kubwa kuzitatua kama kodi zisizokandamiza viwanda, sheria na tozo ambazo zilikuwa zinakwamisha viwanda.
“Sisi na Serikali tunaendelea vizuri sana na masuala haya siyo mepesi kwa sababu inachukua mud asana kujadiliana na kufikia muafaka, lakini kwa dhati kabisa naishukuru serikali kwasababu imekuwa ikitusikiliza kila tunapowasilisha changamoto zetu,” alisema Tenga
Alisema wamefanya Mkutano Mkuu ulioenda sanjari na mjadala kuhusu umuhimu wa kuzingatia masuala ya mazingira na kijamii na uwajibikaji ambapo wanachama wa shirikisho hilo walishiriki kujadili na kutoa mapendekezo yao.
“Nimefurahi sana kuona mjadala ulikuwa mzuri nawashukuru wanachama kwa kuja kwa wingi na tumewasisitiza wenye viwanda kwamba ni muhimu kuzingatia masuala ya mazingira kwani ni ajenda ya dunia kutunza mazingira,” alisema
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Viwanda, Fatma Khamis alipongeza CTI kwa kufikisha miaka 31 tangu kuanzishwa kwake huku ikiendelea kuwa imara na kuwa na sauti kubwa kwa wenye viwanda.
Alisema wenye viwanda wanatakiwa kuzalisha bidhaa kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira, mila na desturi za watanzania na kuhakikisha wazawa wananufaika na uwekezaji wao hapa nchini.
“Hivi sasa ajenda ya mazingira ni ya dunia nzima kwa hiyo nawashauri kila mnachofanya muangalie kama mazingira yetu yanakuwa salama kwasababu bila kutunza mazingira tutaangamiza kizazi kijacho,” alisema
“Nawapongeza CTI kwa kuendelea kuwa imara kwa miaka 31 ya uhai wake, siyo rahisi kwa taasisi kama hizi kuwa imara kwa miaka mingi kiasi hicho kwasababu tunashuhudia nyingi zinakufa kwa changamoto mbalimbali kama ukosefu wa fedha na migogoro lakini hawa wasimama imara mpaka sasa,” alisema
Fatma alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, (SMZ) nay a Muungano zitaendelea kuimarisha mazingira ya kufanya biashara ili kuvutia uwekezaji wa ndani ya nchi na wale wanaotoka nje ya nchi.
Alisema mfano wa dhamira hiyo ni kamati iliyoundwa hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan kwaajili ya kuangalia mfumo wa kodi na kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha.
“Kupitia blue print tumeangalia changamoto mbalimbali za biashara kama mlolongo wa leseni amabzo mwekezaji anatakiwa kuwa nazo kabla ya kuanza uwekezaji, kwa hiyo kuna changamoto nyingi zimeshafanyiwa tathmini,” alisema Fatma
“Mmeona hata namna Rais Samia anavyosafiri mataifa mbalimbali duniani kutafuta wawekezaji na safari zimeshaanza kulipa kwasababu wote ni mashuhuda wa namna wawekezaji kutoka nje ya nchi wanavyozidi kumiminika hapa nchini,” alisema
More Stories
Waziri Mavunde:Benki Kuu yanunua tani 2.6 za Dhahabu nchini
Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25