Na Penina Malundo,Timesmajira
SERIKALI imesema kuwa imetenga kiasi cha Sh. Milioni 66 kwaajili ya kuwafundisha watumishi na wataalam wa masuala ya usonji katika Chuo cha Afya cha Muhimbili ili kuongeza idadi ya Wataalam watakaowasaidia watoto wenye tatizo la Usonji nchini kupatiwa matibabu kwa urahisi.
Ameyasema hayo jana jijini Dar es salaam ,Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya,Dkt. Hamad Nyembea katika hafla iliyoandaliwa na Taasisi ya Lukiza Autism Foundation iliyowakutanisha wadau mbalimbali katika Chakula cha usiku kwa lengo la kufanya harambee ya kuchangisha fedha kiasi cha Shilingi milioni 100 kwa ajili ya kuwasaidia watoto walio na changamoto ya usonji katika suala la elimu na matibabu.
Amesema ugonjwa wa usonji ni miongoni mwa magonjwa yanayoathiri mfumo wa fahamu wa mtoto ambapo huambatana na kuwa na changamoto kwenye njanja zote za makuzi na mahusiano na watoto wenzake na watu wengine katika jamii.
“Tatizo la Usonji ni tatizo la kibaiolojia ambalo humkumba mtoto akiwa ndani ya tumbo la mama yake na tatizo hilo hujidhihirisha zaidi katika hatua zake za ukuaji na wanamtambu ni jamii za mabibi au mababu hivyo ni vyema elimu hiyo ikaenea zaidi ili kusaidia mtoto anapofikia umri wa miaka mitatu awe tayari ameshaanza kliniki ya mazoezi tiba,”amesema na kuongeza
“Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa Dunia nzima kati ya watoto 100 wanaozaliwa kila mwaka mmoja huzaliwa akiwa na usonji ( autism) huku Bara la Afrika watoto 140 mmoja huzaliwa akiwa na hali ya usonji na changamoto kubwa iliyopo ni uwelewa mdogo wa kuanza kuwatambu na kuwahudumia mapema ,”amesisitiza.
Aidha amesema kwa Tanzania takwimu zimeonyesha kuwa watoto Milioni 2 wanaozaliwa kila mwaka ,watoto 14000 huzaliwa wakiwa na hali ya usoji na kwenye vituo vya huduma za afya na shuleni zinaonesha kuwa takribani watoto 2000 tu ndio wanaopatiwa huduma.
Dkt.Nyembea amesema kutokana na uwepo wa tatizo hilo, Wizara ya Afya imeimarisha huduma za Afya ya Akili pamoja na Huduma za Utengamao ili kuweza kuongeza ufanisi kwenye huduma hizo.
Kwa upande wake,Mkurugenzi wa Elimu Maalum wa Wizara ya Sayansi Elimu na Teknolojia, Dkt Magrethy Matonya,amesema watoto wenye Usonji wanavipaji tofauti tofauti wakipatiwa mazingira wezeshi mapema hivyo wameanza na
Mkoa wa Dar es salaam kisha mikoa mingine bara na visiwani katika kuwasaidia kutoa uwelewa wa kutosha kuhusiana na watoto hao.
Amesema watoto hao wanahaki ya kupata haki ya msingi ya elimu kama watoto wengine siyo kutengwa na kunyanyapaliwa.
“Kwa mwaka huu wa fedha 2024 – 2025,Serikali imetoa fursa kwa baadhi ya walimu kusoma somo la Elimu Jumuishi kama somo la lazima na watasoma kwa miaka miwili kwa mwaka 2026 – 2027, hii itasaidia kupata walimu wengi zaidi ambao ni jumuishi watakowafundisha watoto hao
“Hii imekuja baada ya serikali kuona walimu wa watoto hao ni wachache huku wazazi wakiwapeleka shule wanarudishwa nao kwa kuelezwa kuwa walimu ni wachache,”amesema
Kwa upande wake Mwanzilishi wa Asasi ya kiraia Lukiza Foundation,Hilda Nkabi amesema taasisi hiyo inalekea kufikia miaka mitano tangu kuanzishwa kwake na wana mradi walioita ustawi ambapo wanatarajiwa kufika mashuleni kuwafundisha walimu namna ya kuwafahamu wanafunzi wenye tatizo la usonji.
Amesema wapo watoto wengine ambao wanafundishwa katika shule mbalimbali huku wakiwa wanapatiwa adhabu na kuonekana kuwa watundu kumbe wanakuwa na changamoto ya usonji.
Nkabe amesema mbali na harambee hiyo ya kuchangisha fedha kiasi cha Shilingi milioni 100 kwa ajili ya kuwasaidia watoto walio na changamoto ya usonji pia wamezindua Usajili wa mbio za Marathoni zitakazofanyika Mwaka 2025 ambapo kila mshiriki anapaswa kulipa tsh. 40000 lengo ikiwa ni muendelezo wa ukusanyaji wa fedha kwa ajili ya kusaidia watoto wenyewe usonji kufikia malengo yao.
Katika harambee hiyo ya the 3rd Autism Awareness Fundraising Gala Dinner,
Fedha iliyokusanywa ni jumla ya kiasi ya sh.81,600,000 kiasi ambacho kilichangishwa kabla na wakati wa hafla hiyo.
More Stories
Mavunde mgeni rasmi uzinduzi wa mnada wa madini ya vito Desemba 14,Mirerani
GST,BGS zafanya majadiliano namna ya kuanzisha mashirikiano katika tafiti na kujengeana uwezo
Utekelezaji wa Mou Tanzania,Burundi waanza rasmi