Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya
JAMII nchini imetakiwa kuwajumuisha watu wenye ulemavu katika shughuli za kila siku kwa wakati pamoja na kuwapa nafasi za ajira ili kuonesha uwezo wao na vipaji vyao walivyonavyo.
Imeelezwa kuwa ili kujenga jamii jumuishi kila mtu kuna kitu Mungu amempa ambacho ni mchango wake katika jamii,hivyo mtu mwenye ulemavu akipewa nafasi ya kuingiza mchango wake kutakuwa na matokeo makubwa.
Hayo yamesemwa Desemba 3,2024 na Mkurugenzi wa Shirika lisilo kuwa la kiserikali linalojishughulisha na watu wenye ulemavu(CST),Noela Msuya wakati wa maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu Duniani Iliyofanyika katika hotel ya Gr City Jijini hapa .
Msuya amesema kuwa siku ya watu wenye ulemavu ni muhimu kupeleka ujumbe kwa jamii kuhusu masuala mazima yanayohusiana na watu wenye mahitaji maalum lakini zaidi kupeleka ujumbe wa uwezo,vipaji,vipawa walivyonavyo katika kuviendeleza.
Consolata Mng’ong’o kutoka Dawati la Jinsia na Watoto ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya,amesema kuwa wameweza kutoa elimu kwa jamii lakini bado watoto wenye ulemavu wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili.Licha ya kufanyiwa vitendo hivyo bado wazazi wamekuwa wakishindwa kuwathamini kama ni watoto kama walivyo wengine.
“Kama mtoto kuwa na ulemavu wa aina yeyote ile usimfiche ndani mtoe nje ,mpeleke sehemu za michezo akacheze,pia mpeleke shule kama hizi apate elimu leo hii unamficha ndani tayari ana shida ambayo amezaliwa nayo,vile unavyomweka ndani unampa changamoto nyingine ya kumpa shida ya kujiona yeye ni nani,”amesema Mng’ong’o.
Aidha amesema Child Support Tanzania wamekuwa wakiwasomesha vijana wenye ulemavu ambao,wamerudi kwenye kituo na kuwalea watoto wenye ulemavu, hivyo watoto hao waliopo nyumbani wakifichuliwa mwisho wa siku watafanya vitu ambavyo jamii itashangaa.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, George Emmanuel,amewataka wazazi na walezi kutowaficha watoto wenye ulemavu kwani wana uwezo mkubwa,hivyo jamii na wazazi kuendelea kuwaibua watoto wenye ulemavu.
Emmanuel amesema kuwa serikali ya Mkoa wa Mbeya, iliona umuhimu wa wanafunzi wenye ulemavu kwa kuanza ujenzi wa shule maalum ya kisasa Tanzania, ambayo itajengwa eneo la TBC Iwambi ambayo itakuwa jumuishi kwa maana asilimia 80 , na asilimia 20 kwa wale wengine kusaidia wenye ulemavu.
Shule hiyo ambayo itazingatia mahitaji yote ya wanafunzi wenye mahitaji maalum kuanzia miundombinu na kuzingatia aina ya elimu ambayo wanatakiwa kupatiwa.
Aidha alishukuru uongozi wa Child Support Tanzania,kutochoka kuwaibua watoto wenye ulemavu na kuwa serikali ipo bega kwa bega katika kuwasaidia ili kuweza kusaidia juhudi za kuendeleza kusaidia watoto wenye mahitaji maalum.
More Stories
Wanaoficha watoto wenye ulemavu kusakwa
Mawakili Tabora walaani kuziwa kutekeleza majukumu
RC Mrindoko:Ufyekaji wa mahindi Tanganyika si maelekezo ya serikali