December 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bilioni 8.6, kutumika kwa ruzuku nishati safi ya kupikia

Judith Ferdinand,Timesmajira Online,Mwanza

Serikali imekusudia kutumia kiasi cha bilioni 8.6 kwa ajili ruzuku kwenye nishati safi za kupikia ambayo ni mitungi ya gesi 452,000,ya kilo 6 na vifaa vyake kwa ajili ya kupikia vitakavyouzwa kwa Tsh 20,000, pekee kwa wakazi wa vijijini na maeneo ya pembezoni mwa miji nchini hapa.

Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia za mwaka 2023, zinasema idadi ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia,imekuwa ikiongezeka kwa kiwango kidogo kutoka asilimia 1.5 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 6.9, mwaka 2021, ambapo kiwango hicho ni chini ya kiwango cha wastani cha Dunia cha asilimia 71 kwa mwaka 2021.

Hayo yamebainishwa Desemba 2,2024 na Mhandisi Mwandamizi wa Wakala wa Nishati Vijijini(REA),Deusdedith Malulu,wakati akitoa taarifa kwa Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza wa utekelezaji wa mradi wa ugawaji mitungi ya gesi ya kupikia ya uzito wa kilo 6, kwa Mkoa wa Mwanza.

Mhandisi Malulu,amesema mradi wa mitumgi ya gesi ya kilo sita,yenye vifaa vyake vyote kwa ajili ya kupikia,itauzwa kwa bei ya ruzuku badala ya kuuzwa kwa Tsh.40,000 itauzwa kwa Tsh.20,000.Ambapo ruzuku hiyo imetolewa na
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini(REA),kwa lengo la kufikia asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034.

Kupitia mradi huo, utahakikisha wananchi wanapata nishati safi ya kupikia kwa bei nafuu na kwa utoshelevu,kwa nchi mzima,ambapo kwa Mkoa wa Mwanza wanatarajia mitungi na majiko yake takribani 19,530,itauzwa kwa bei ya ruzuku.

“Majiko 3,255, kwa kila Wilaya zilizopo mkoani Mwanza yatauzwa kwa Tsh.20,000.Ambapo REA imeingia mkataba na mtoa huduma Lake Gas Limited ambaye atahudumia Wilaya za Mkoa huu,kwa bei hiyo katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa Miji,”.

Sanjari na hayo,amesema Serikali imetoa ruzuku ya asilimia 75 katika mradi wa mitambo ya nishati ya jua (solar system) unaofungwa kwenye bati,ambao utawanufaisha wananchi wa maeneo ya visiwani, kwa kununua mtambo huo kwa bei ya ruzuku ya 150,000 hadi 200,000 badala ya ya makadirio ya 600,000.

“Mwanza ni eneo ambalo linavisiwa vingi,takribani ‘system’,8,575,zitauzwa kwa bei ya ruzuku katika maeneo ya visiwa mbalimbali na vilivyopo katika Ziwa Victoria,”.

Aidha amesema, Serikali inatoa mikopo wa kiasi cha milioni 133, kwa wananchi ili waweze kujenga vituo vidogo vya mafuta maeneo ya vijijini,ambapo kumekuwa na changamoto ya uuzwaji wa mafuta kwa njia ambayo si salama ya kwenye chumba na madumu.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Arch.Chagu Nghoma,amesema majiko hayo yatauzwa kwa wananchi wa kawaida vijijini na mjini.Kwani imeonekana umuhimu wa kila familia kwa asilimia kubwa iweze kupata majiko ya gesi na huduma ya nishati hiyo safi ya kupikia kama ilivyokusudiwa na Serikali.

“Maelekezo ni kwamba kila familia moja utapata jiko moja,hivyo watatumia kitambulisho cha Taifa(NIDA),ili kusiwepo mtu kati ambaye atanunua majiko hayo kwa bei ya ruzuku na kisha kuwauzia wananchi kwa bei ya juu,kwani Serikali imetoa majiko haya kwa ruzuku,”.

Mkoa umepokea mradi huo kwa mikono miwili,ili wananchi waweze kunufaika,na itatolewa elimu kwao na waweze kujua namna bora ya kutumia gesi hiyo.

Hata hivyo amesema,kuhusu mradi wa nishati ya jua,utasaidia Mkoa huo ambao una visiwa vingi sana huku wananchi wa maeneo hayo kupata umeme wa gridi ya taifa ni kazi ngumu.